MKUU wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya amedai kuwa Mbunge
wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige amemwandalia kundi kubwa la vijana, ambao
wamepanga kulipiga mawe gari lake, kutokana na msimamo wake aliouweka katika
ugawaji wa chakula cha msaada kwa waathirika wa mvua kubwa ya mawe, iliyoua
zaidi ya watu 46 katika kijiji cha Mwakata, wilayani hapa.
Hata hivyo, Maige amekana, huku akimtaka Mkuu huyo wa wilaya
kuacha kutafuta kisingizio cha kushindwa kusambaza chakula kwa wakati kwa
waathirika.
Mpesya, Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, alisema hayo juzi
wakati akizungumza na gazeti hili katika eneo la tukio.
Alisema suala la waathirika hao, limegeuzwa kuwa la kisiasa
na baadhi ya viongozi wakubwa wa kisiasa kwa kuhamasisha kudai misaada ya
vyakula kinyume na taratibu uliowekwa na Serikali.
Pia, wanasiasa hao wametuhumiwa kudiriki kuhamasisha
waathirika kuzuia mabasi kwa kulala barabarani ili kukosesha huduma ya
wasafiri, ambao hawana uhusiano na tukio lililotokea Mwakata.
Hali hiyo imekuwa ikilalamiki wa na wasamaria, ambao
wamekuwa wakimiminika kila siku kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao.
Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa waliolala barabarani
siyo waathirika, bali ni kundi la vijana kutoka katika vijiji jirani vya
Kagongwa na Isaka, wanaodaiwa kuandaliwa na Maige.
Akizungumzia tukio hilo, Maige alikanusha kuhusika na kusema
maelezo ya mkuu huyo wa wilaya, siyo ya kweli na kwenda mbali zaidi, akisema
anawaumiza kisaikolojia waathirika wa mafuriko kwa kuwachelewesha msaada.
“Kitendo alichokifanya mkuu wa wilaya cha kuwapiga mabomu
waathirika, nacho ni sisi wanasiasa, kuna wanawake waliokuwa na watoto wao
baada ya mabomu kupigwa na wanawake hao kulazimika kuwakimbia, je, anajua
waliko? Asikae kuimba nyimbo za siasa na kukwepa majukumu yake”, alisema Maige
ambaye amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Alipoulizwa kuhusu tukio hili la waathirika kulala
barabarani, Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Justus Kamugisha alisema Polisi
walifika kuondoa waathirika na wananchi waliokuwa siyo waelewa na jeshi hilo
halikutumia nguvu.
Kuhusu waliolala barabarani, Kamanda alisema si waathirika
wa tukio hilo, bali ni vijana kutoka sehemu mbalimbali za vijiji vya Kagongwa
na Isaka.
“Waathirika wa tukio hilo kwa kupatwa na maafa makubwa kama
hayo na kufiwa na ndugu zao, tulishuhudia kuna familia zingine zimepoteza
watoto watano, hivi inaingia akilini na nguvu utaipataje ya kwenda kulala
barabarani ili uishinikize Serikali kukupatia misaada, hao ni watu ambao
hawawahurumii waliopatwa na matatizo hayo,” alisema Kamanda Kamugisha.
Tangu kutokea kwa maafa hayo, kumekuwa na mvutano baina ya
wanasiasa na viongozi wa Serikali kuhusu utoaji wa chakula kwa waathirika, hali
iliyosababisha baadhi yao kutoleana lugha chafu mbele ya wananchi.
Wakati huo huo, Benki ya NBC Tawi la Kahama imetoa msaada wa
vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 5 kwa waathirika wa maafa
hayo, yaliyotokana na mvua ya mawe iliyonyesha hivi karibuni katika Kijiji cha
Mwakata wilayani hapa na kusababisha vifo vya watu 46.
Misaada hiyo ilikabidhiwa juzi na Meneja wa NBC Tawi la
Kahama, Martin Nkanda ambaye alisema NBC inaungana na wasamaria wema
waliojitolea misaada mbalimbali kwa waathirika wa maafa hayo.
Benki hiyo imekabidhi unga wa sembe mifuko 100, kilo 200 za
maharage, ndoo 50 za mafuta ya kula yenye ujazo wa lita kumi kumi, chumvi,
katoni 15 za sabuni za kufulia, shuka 100, mablanketi 100 na katoni 15 za
madaftari kwa ajili ya wanafunzi walioathiriwa vifaa vyao vya masomo.
No comments:
Post a Comment