Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, October 29, 2015

David Kafulila Akwama Kigoma Kusini, CCM yaibuka Kidedea


Mgombea ubunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila ameanguka katika matokeo yaliyotangazwa jana jioni dhidi ya mpinzani wake wa CCM, Hasna Mwilima.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Uvinza ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini, Ruben Mfume amesema Kafulila alipata kura 33, 382 huku mpinzani wake wa CCM akipata kura 34, 453.

Akizungumzia kuchelewa kutangazwa kwa matokeo katika jimbo hilo, Mfume amesema ni kutokana na kuwepo malalamiko kadhaa toka kwa wagombea wote wawili wa CCM na NCCR-Mageuzi ambapo mgombea wa CCM alikuwa anataka kura zihesabiwe upya.



Mfume amesema, mgombea wa CCM (Mwilima) alitoa madai kuwa fomu zake za kurekodi matokeo zilionekana zimefutwafutwa kwenye kata nyingi, hali iliyompa wasiwasi kuwa huenda matokeo yake kwenye Kata hizo yamechezewa.

Katika madai mengine, Mfume amesema Mwilima amedai fomu zake za matokeo kwenye kata nyingi zilionekana kusainiwa na mawakala wa chama cha mpinzani wake (NCCR-Mageuzi), hali iliyomuondolea imani ya usahihi takwimu  za matokeo hayo.

Kwa upande wake, Kafulila amepinga hoja ya kutaka kura zihesabiwe upya kwa madai kuwa hakuwa na imani na waliopewa dhamana ya kuzilinda kura zao baada ya kuhesabiwa akidai walinzi pamoja wa mkurugenzi huyo ni mawakala wa CCM katika uchaguzi.

Kafulila amesema kutokana na uwakala wao kwa CCM, walinzi pamoja na mkurugenzi huyo walikuwa na uwezo wa kufanya lolote baada ya zoezi la kuhesabu kura kukamilika na kubadili matokeo ili kuisaidia CCM kushinda.

Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, Kafulila amesema hakubaliani na hatua ya mgombea wa CCM kutangazwa mshindi kwa kuwa dosari walizolalamikia zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi wala yeye hakuwa ameridhia matokeo hayo yatangazwe.

Matokeo ya udiwani katika jimbo hilo lenye Kata 16 yanaonyesha kuwa, CCM kimeshinda Kata 13, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na ACT-Wazalendo vikijipatia ushindi katika Kata moja kila kimoja.

No comments:

Post a Comment