Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, December 18, 2015

MAKONDA AIBUA UFISADI WA BILIONI 5.7 KINONDONI


MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (pichani) ameamuru kusitishwa mara moja malipo yanayofanywa kwa makandarasi waliojenga barabara tano za ndani ya wilaya hiyo
Amefanya hivyo kwa maelezo kuwa watendaji wa Manispaa hiyo, wameshirikiana na makandarasi hao kuiibia serikali Sh bilioni 5.7. Fedha hizo ni ongezeko ambalo makandarasi hao, wanatakiwa kulipwa baada ya kujenga barabara hizo, ambazo thamani halisi ya ujenzi huo ni Sh bilioni tano.
Lakini, katika hali isiyo ya kawaida, makandarasi hao wanatakiwa kulipwa Sh bilioni 10, ongezeko ambalo ni zaidi ya asilimia 100. 
Akizungumza jana Dar es Salaam, Makonda alisema taratibu za Serikali zinataka kama barabara haikukamilika ndani ya muda uliowekwa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo mvua na sababu zinginezo, mkandarasi anatakiwa kulipwa fedha zaidi ambazo ni asilimia 15 ya thamani ya fedha za mradi.


“Lakini kinachostaajabisha katika miradi hii ya barabara, fedha ambazo zimeongezeka ni zaidi ya asilimia 15, kiasi hiki ni zaidi pia ya asilimia 100, wametumia utaratibu gani kulipa fedha hizi za ziada kwa makandarasi hawa?” Alihoji Makonda.

Alizitaja barabara ambazo watendaji wamezitumia kufisadi fedha za umma kuwa ni ujenzi wa barabara ya Lion kwa kiwango cha lami yenye thamani ya Sh milioni 592.1, lakini nyongeza ya fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 860.1 na hivyo kufanya mradi huo kugharimu Sh bilioni 1.4.

Barabara ya kutoka Biafra hadi Embassy, matengenezo yalikuwa ni Sh milioni 507.9 na fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 487.5 jumla ya malipo kwa mkandarasi ni Sh milioni 994, barabara ya Mabatini thamani ya mradi ilikuwa Sh milioni 655.5 na fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 777.8 na jumla ya mradi kugharimu Sh bilioni 1.4.

Makonda alitaja barabara nyingine zilizojengwa kwa kiwango cha lami zenye ufisadi ni ya Journalism, ambayo ujenzi wake ulikuwa ugharimu Sh bilioni mbili, nyongeza ya fedha katika mradi huo ni Sh bilioni 1.8 na hiyo kufanya mradi huo hugharimu Sh bilioni 3.8, Barabara ya Maandazi ambayo thamani ya mradi ni Sh milioni 799 imeongezwa kiasi cha fedha Sh bilioni 1.2 na hivyo kufanya mradi wote kugharimu Sh bilioni 2.

“Nyongeza hizi zinatia shaka na ni jambo la kushangaza, nimeamuru makandarasi wasiendelee kulipwa fedha hizi na nimetoa siku tano kwa ofisi ya uchunguzi ya mkoa ichunguze malipo haya na mafaili ya miradi hiyo yaletwe ofisini kwangu mara moja,” alisema Makonda.

Alisema ili malipo ya ziada yalipwe, lazima Bodi ya Zabuni ya Wilaya na Bodi ya Mfuko wa Barabara, ziidhinishe malipo hayo.
 
 “Lakini cha kushangaza katika malipo haya, yanayoendelea kufanywa na Manispaa, makandarasi wamelipwa kabla hata bodi hazijatoa ukubali wa malipo haya kufanyika,” alisema.

Alisema Bodi ya Mfuko wa Barabara katika ripoti yao, walikataa fedha hizo za malipo ya zaida zisitolewe. Lakini, alisema fedha hizo zilitolewa na Manispaa kwa makandarasi hao na hiyo inaonesha kwamba kuna mchezo mchafu, umefanywa kati ya watumishi wa Manispaa na makarandasi wenyewe.

Alisema wahusika wakuu katika malipo hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Kitengo cha Manunuzi, Mhandisi wa Barabara wa Manispaa ambao ndio wanatakiwa kutoa maelezo ya kuwepo kwa nyongeza hiyo ya malipo kinyume cha taratibu za Serikali.

“Watu wanadai naingilia kazi za watu, nisipobaini uozo huu kwenye wilaya yangu sifai kuwa mkuu wa wilaya, haiwezekani watu wafisadi fedha za umma kiasi hiki wakati tunakosa hata pesa ya kujenga wodi ya wazazi pale Hospitali ya Mwananyamala,” alisema Makonda.

Alisema ataendelea kupambana, kuhakikisha kwamba kila mwananchi anafaidika na keki ya Serikali ;na sio watu wachache ambao wamepewa dhamana ya kufanya kazi kwenye ofisi za umma wafaidike na keki hiyo.

Barabara hizo ni nje ya barabara zingine, ambazo Makonda mwanzoni mwa mwaka huu aliziundia tume kuchunguza ujenzi wake, ambao walidai ulikuwa chini ya kiwango hali inayofanya mvua zikinyesha barabara hizo zinageuka mahandaki.

Tume hiyo ilibaini ujenzi kuwa chini ya kiwango, lakini mabilioni ya fedha zimetumika katika ujenzi huo. 
 
Ilipendekeza hatua kuchukuliwa kwa wahusika waliohusika kujenga barabara hizo, ambazo mvua ikinyesha zinageuka mashimo.

No comments:

Post a Comment