Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, December 7, 2015

NEC YATAOA TAMKO KUHUSU UCHAGUZI WA WABUNGE ARUSHA MJINI NA HANDENI.


 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu uchaguzi wa wabunge unaotarajiwa kufanyika Tarehe 13/12/2015 katika jimbo Handeni na Arusha Mjini, (kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura Bw.Clarence Nanyaro kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
 Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva(ambaye hayupo katika picha) leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waaandishi wa habari kuhusu taratibu zitakazo tumika katika uchaguzi wa wabunge katika jimbo la Arusha na Handeni.
Na Jacquiline Mrisho

 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza siku ya kupiga kura kwa baadhi ya majimbo ambayo uchaguzi wake ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametaja siku hiyo ya uchaguzi itakuwa Disemba 13, mwaka huu.

“Natoa rai kwa Wananchi wote waliojiandikisha kama wapiga kura katika Majimbo na Kata husika kujitokeza katika vituo walivyojiandikishia ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka” amesema Lubuva.

Jaji Lubuva aliyataja majimbo hayo ambayo wananchi watapiga kura za kuchagua Wabunge kuwa ni Majimbo ya Arusha Mjini na Handeni Mjini ambapo uchaguzi wa Madiwani katika kata za Mvomero, Ipala na Nyamwilolewa nao utafanyika siku hiyo.
Aidha, Jaji Lubuva alisisitiza kuwa, taratibu zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 mwaka ndizo zitakazotumika kwenye uchaguzi kwenye majimbo hayo na kata hizo.

Kwa ufupi, Jaji Lubuva alikumbushia baadhi ya taratibu hizo zikiwemo za mpiga kura kubeba kadi yake ya kupigia kura pindi aendapo kupiga kura, mawakala wa vyama vya siasa lazima wawepo kwenye kila kituo na pia Maafisa Uchaguzi kufungua kituo na kufunga kwa muda uliopangwa na Tume.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, uchaguzi wa Wabunge na Madiwani wa Majimbo 7 pamoja na Kata 35 ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vifo na vurugu.

No comments:

Post a Comment