Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, December 7, 2015

RAIS DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI AOKOA SH1TRILIONI KWA MUDA WA SIKU 30 ZA KUWA MADARAKANI


Rais John Magufuli jana ametimiza mwezi mmoja tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo huku akiweka rekodi ya kuokoa kiasi cha Sh997.4 bilioni (karibu Sh 1trilioni) ambazo zilikuwa zitumike kwa matumuzi yasiyo ya lazima, na ukwepaji kodi.

Sh997.4 bilioni zilizookolewa zitaweza kutumika kununua magari ya wagonjwa, kujenga zahanati, kujenga barabara za lami, kununua madawati, kujenga vyumba vya madarasa, kuchimba visima, kununua mashine za uchunguzi wa magonjwa, magari ya wanafunzi, pikipiki kwa maofisa kilimo, mikopo ya elimu ya juu au kujenga viwanja vya michezo kadri Serikali itakavyoelekeza.

Dk Magufuli aliapishwa Novemba 5 katika hafla iliyofana na alianza kazi ya kutafuta na kuziba mianya ya upotevu wa fedha Novemba 6 alipotembelea Hazina. Katika mazungumzo ya watendaji wa wizara hiyo Rais Magufuli alipiga marufuku safari zote za nje na kwamba zitakuwa zinaruhusiwa kwa kibali maalumu.


Novemba 7 alitembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako aliagiza mashine za MRI na CT-Scan zitengenezwe na aliagiza Sh3 bilioni zitolewe kugharimia matengenezo kati ya Sh7 bilioni zilizokuwa zinahitajika.

Novemba 19, Dk Magufuli aliwasilisha bungeni jina la Kassim Majaliwa, mbunge wa Ruangwa kwamba ndiye alimpendekeza kuwa Waziri Mkuu. Baada ya jina kupitishwa na Bunge, Novemba 20 Kassim Majaliwa aliapishwa.

Jioni alilihutubia Bunge akionyesha mwelekeo wa Serikali yake ya awamu ya tano. Katika hotuba hiyo iliyowasisimua wabunge na hata wananchi waliosikiliza kupitia televisheni na redio, Dk Magufuli aliahidi kupambana na mafisadi, kubana matumizi, kuhimiza utendaji kazi, kuinua uchumi na kulinda amani na utulivu.

Baada ya hapo Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa wamekuwa wakitembelea maeneo muhimu kwa uchumi wa nchi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bandari na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)

Utendaji huo wa Serikali wa Magufuli ndani ya mwezi moja na kipindi kabla hajaunda baraza la mawaziri, umetazamwa na jamii kuwa ni mbinu ya kusafisha nchi na kutengeneza mazira safi ili mawaziri watakaoteuliwa wafuate kasi hiyo.

Fedha zilizookolewa

Kwa kuzingatia ripoti ya matumizi ya fedha za safari zilizolipwa kama nauli na posho kwa kipindi cha kati ya mwaka 2013 na 2015 kiasi hicho ni pamoja na Sh356.3 ambazo zingeweza kutumika kwa safari hizo. Dk Magufuli aliagiza kwamba baadhi ya shughuli zitafanywa na mabalozi wa Tanzania walioko nje.

Novemba 19 alipozindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma, Dk Magufuli aliagiza Sh225 milioni zilizokuwa zimekusanywa kwa ajili ya hafla ya wabunge, zipelekwe kununua vitanda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Fedha hizo zilinunua vitanda 300, magodoro 300, mablanketi 1675, na viti vya magurudumu 30.

Pia, katika hotuba yake bungeni, Dk Magufuli alirejea uamuzi wake wa kufuta safari za nje kwa watendaji wa Serikali na kueleza safari hizo zimeigharimu Serikali Sh356.3bilioni ambazo zingeweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 400.

Novemba 23, Dk Magufuli alitangaza kufutwa kwa maadhimisho ya Siku ya Uhuru Desemba 9 na akaagiza Sh4 bilioni ambazo zingetumika zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Morocco kwenda Mwenge. Kazi hiyo imeanza.

Novemba 25, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitangaza kufutwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani na akaelekeza kwamba fedha zilizopangwa kwa ajili ya sherehe hizo zitumike kununua dawa za kufubaza makali ya ukimwi (ARVs).

Novemba 27, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea bandarini na kubaini makontena 349 ambayo yalitolewa bandarini bila kulipiwa ushuru na kuifanya Serikali kukosa mapato ya Sh80 bilioni.

Tayari wenye makontena hayo wameanza kulipia na jana TRA ilitangaza kukusanya Sh6.3 bilioni kati ya hizo Sh80 bilioni. Katika ziara yake nyingine ya kushtukiza Desemba 3 Majaliwa alibaini makontena 2,431 yalitolewa bila kulipiwa kodi. Ikiwa makontena hayo yangelipiwa kodi viwango sawa na yale 349 Serikali ingepata Sh557.2 bilioni.

Desemba 3, Dk Magufuli alifanya mazungumzo na jumuiya ya wafanyabiashara nchini na akawataka wote ambao waliondoa mizigo yao bandarini bila kulipa kodi, wajitahidi kulipa katika kipindi cha siku saba kuanzia juzi vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Makontena ni shida

Desemba 1, makontena mengine tisa yalikamatwa na TRA eneo la Mbezi, Tangibovu yakiwa yametoroshwa bila kulipuiwa ushuru wa Sh58 milioni. Jumla ya Sh637.2 zimeokolewa kutokana na mkakati wa kukusanya fedha kutoka kwenye makontena 2,431 pamoja na 349 na hayo tisa.

Matumizi ya Sh 997.4 bilioni

Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikikwama kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kutokana na kukosa fedha. Dk Magufuli alikiri juzi kuwa hakuna fedha za maendeleo zilizokuwa zimetolewa kwa wizara zote katika mwaka huu wa fedha wa 2015/16, lakini baada ya miezi sita juzi ndiyo zimetolewa Sh120 bilioni.

Dk Magufuli hakusema Serikali imepata wapi fedha hizo, lakini huenda ni sehemu ya fedha ambazo ameokoa katika kipindi cha mwezi mmoja.

Kama fedha hizo zingeelekewa katika ujenzi wa barabara, na kwa kuzingatia kilomita moja inajengwa kwa Sh1 bilioni, fedha hizo zitaweza kujenga karibu au zaidi ya kilomita 1,000, ambao ni umbali kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma au Dar es Salaam mpaka Tunduma.

Aidha, Sh997.4 bilioni zingeweza kununua magari 3,325 ya kubebea wagonjwa kwa gharama ya Sh300 milioni kwa kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata magari 133 ya aina hiyo.

Pia, zahanati moja yenye vifaa vyote muhimu ujenzi wake unagharimu kati ya Sh600 milioni na Sh700 milioni. Hivyo, fedha hizo zingeweza kujenga zahanati 1,425 yaani kila mkoa ungepata zahanati 57.

Vilevile, wakati maelfu ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wanasoma kwa kukaa chini kutokana na kukosa madawati, Sh997.4 bilioni zitaweza kutengeneza madawati yenye miguu ya chuma 33,249,142 kwa gharama ya Sh30,000 kwa kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata madawati 1,329,966.

Pengine, fedha hizo zinaweza kujenga vyumba vya madarasa 132,996 kwa bei ya Sh7.5 milioni kwa darasa moja, hatua ambayo itawezesha kujengwa kwa vyumba vya madarasa 5,319 kila mkoa nchini.

Kipimo maarufu cha CT-Scan ambacho ufanyaji wake wa kazi unasuasa Muhimbili kwa muda mrefu, kinauzwa kwa wastani wa Sh900 milioni, hivyo, Sh997.4 bilioni zitaweza kununua mashine 1,108 ambazo zingesambazwa na kila mkoa ukapata mashine 44.

Gharama za kuchimba kisima kifupi ni kati Sh1 milioni na Sh3 milioni kulingana na jiografia ya eneo husika, hivyo Sh997.4 bilioni zitaweza kuchimba visima 332,491; kila mkoa ukapata visima 13,299.

Pia, kwa kuwa Serikali inahimiza uboreshaji wa sekta ya kilimo, Sh997.4 bilioni zitaweza kununua pikipiki 332,491 na kugawiwa kwa maofisa kilimo kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa kilimo vijijini na kila mkoa ungepata pikipiki 13,299.

Kama fedha hizo zitaelekezwa kwenye mikopo ya elimu ya juu, zitaweza kugharamia wanafunzi 249,368 wa mwaka wa kwanza kwa asilimia 100 kwa wastani wa Sh4 milioni kwa kila moja kwa ajili ya chakula, malazi na ada.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Joyce Mmasi na Peter Saramba

No comments:

Post a Comment