Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, December 7, 2015

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUSAINI KIAPO CHA AHADI NA UADILIFU

Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeanza rasmi kutekeleza Ahadi ya Uadilifu kwa watumishi wa Umma nchini .
Akiongea na vyombo vya habari leo, Katibu Mkuu Hab  Mkwizu amesema utekelezaji huo umeanza rasmi Desemba, 2015 ambapo kila Mtumishi wa Umma ataweka saini  ya kiapo  kwa kuzingatia  taratibu zilizowekwa na  mazingira ya taasisi husika.
“Utaratibu wa Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Watumishi wa Umma umetolewa kupitia waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma  Na. 2 wa mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi, Watumishi wa Umma na sekta binafsi wa tarehe 1 Agosti, 2015.” alisema Mkwizu.
Mkwizu aliongezea kwa kusema, uanzishwaji wa Ahadi na Uadilifu  ni muendelezo wa uundwaji wa vyombo vya kusimamia maadili baada ya ongezeko kubwa la ubadhirifu, utoro sehemu za kazi na kushuka kwa nidhamu katika kipindi cha miaka ya themanini na tisini.
Alivitaja vyombo vingine ambavyo vilianzishwa kusimamia ahadi na 
uadilifu kuwa ni Sekretariate ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).


Mkwizu alivitaja vipengele ambavyo mtoa ahadi anatakiwa kuvitamka ni, kuwa mzalendo wa nchi yake na kutii Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kuhudumia Umma na watumishi wenzake kwa heshima, kutimiza wajibu wa kutoa huduma bora kwa umma, kutoa huduma bora kwa usawa kwa watu wote na kutofanya ubaguzi wa dini, siasa, kabila, udugu, ukanda, jinsia, urafiki au hali ya mtu.
Vipengele vingine ni kutumia rasilimali za Umma kwa manufaa ya Umma, kutotoa siri za Serikali au mteja kwa watu wasiohusika isipokuwa kwa maslahi ya Umma, kufanya kazi kwa nidhamu ya hali ya juu, kutoomba kushawishi, kutoa wala kupokea rushwa na kutotumia madaraka kwa manufaa binafsi ya ndugu, rafiki au jamaa.
Aidha, Mkwizu ametoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Ahadi na Uadilifu unakamilika  ifikapo tarehe 31/12/2015 na kuwasilisha Ofisi ya Rais – UTUMISHI kabla ya tarehe 25/02/2016 na utekelezaji wake kuwa kila ifikapo Juni 30 ya kila mwaka. 
Fomu za Ahadi ya Uadilifu zinapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Rais – UTUMISHI yenye anwani www.utumishi.go.tz.

No comments:

Post a Comment