Rais  Jakaya Mrisho Kikwete leo amewaapisha mjumbe wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu John Mkwawa pamoja na Katibu wa Tume ya Kurekebisha sheria Bi.winfrida Beatrice Korosso katika hafla iliyofanyika ikulu jijini Dar es Salaam leo asubuhi. Pichani  juu ni mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu John Mkwawa(8724)  na chini ni Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Bi.Winfrida Beatrice Korosso(8734) Wakila kiapo mbele ya Rais leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Novemba 26, 2012 amewaapisha Majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Katika sherehe iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Rais Kikwete amewaapisha Jaji Bethuel  M.K. Mmilla na Jaji Ibrahim Juma kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani.
 Rais Kikwete aliwateua Majaji hao tokea Oktoba 25, mwaka huu wa 2012, na kabla ya uteuzi wake, Jaji Bethuel M.K. Mmilla alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu kwa miaka kumi tangu Juni 02, 2002. Vile vile, Jaji Mmilla amekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kwenye vituo vya Sumbawanga, Arusha na Mbeya.
Naye Jaji Ibrahim Juma kabla ya uteuzi wake alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria tangu mwaka 2007 na pia Jaji wa Mahakama Kuu tangu Juni, 2009. Pia amewahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kati ya mwaka 2003 na mwaka 2006.
Katika hafla tofauti iliyofanyika hapo hapo Ikulu leo, Rais Kikwete amemwapisha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa John Mkwawa kuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na amemwapisha Bi. Winfrida Beatrice Korosso kuwa Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
     ……..Mwisho………..
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
26 Novemba, 2012