Pages

Monday, March 9, 2015

DC NA MBUNGE WAINGIA KWENYE BIFU!!!

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya amedai kuwa Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige amemwandalia kundi kubwa la vijana, ambao wamepanga kulipiga mawe gari lake, kutokana na msimamo wake aliouweka katika ugawaji wa chakula cha msaada kwa waathirika wa mvua kubwa ya mawe, iliyoua zaidi ya watu 46 katika kijiji cha Mwakata, wilayani hapa.


Hata hivyo, Maige amekana, huku akimtaka Mkuu huyo wa wilaya kuacha kutafuta kisingizio cha kushindwa kusambaza chakula kwa wakati kwa waathirika.
Mpesya, Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, alisema hayo juzi wakati akizungumza na gazeti hili katika eneo la tukio.
Alisema suala la waathirika hao, limegeuzwa kuwa la kisiasa na baadhi ya viongozi wakubwa wa kisiasa kwa kuhamasisha kudai misaada ya vyakula kinyume na taratibu uliowekwa na Serikali.
Pia, wanasiasa hao wametuhumiwa kudiriki kuhamasisha waathirika kuzuia mabasi kwa kulala barabarani ili kukosesha huduma ya wasafiri, ambao hawana uhusiano na tukio lililotokea Mwakata.
Hali hiyo imekuwa ikilalamiki wa na wasamaria, ambao wamekuwa wakimiminika kila siku kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao.
Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa waliolala barabarani siyo waathirika, bali ni kundi la vijana kutoka katika vijiji jirani vya Kagongwa na Isaka, wanaodaiwa kuandaliwa na Maige.
Akizungumzia tukio hilo, Maige alikanusha kuhusika na kusema maelezo ya mkuu huyo wa wilaya, siyo ya kweli na kwenda mbali zaidi, akisema anawaumiza kisaikolojia waathirika wa mafuriko kwa kuwachelewesha msaada.
“Kitendo alichokifanya mkuu wa wilaya cha kuwapiga mabomu waathirika, nacho ni sisi wanasiasa, kuna wanawake waliokuwa na watoto wao baada ya mabomu kupigwa na wanawake hao kulazimika kuwakimbia, je, anajua waliko? Asikae kuimba nyimbo za siasa na kukwepa majukumu yake”, alisema Maige ambaye amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Alipoulizwa kuhusu tukio hili la waathirika kulala barabarani, Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Justus Kamugisha alisema Polisi walifika kuondoa waathirika na wananchi waliokuwa siyo waelewa na jeshi hilo halikutumia nguvu.
Kuhusu waliolala barabarani, Kamanda alisema si waathirika wa tukio hilo, bali ni vijana kutoka sehemu mbalimbali za vijiji vya Kagongwa na Isaka.
“Waathirika wa tukio hilo kwa kupatwa na maafa makubwa kama hayo na kufiwa na ndugu zao, tulishuhudia kuna familia zingine zimepoteza watoto watano, hivi inaingia akilini na nguvu utaipataje ya kwenda kulala barabarani ili uishinikize Serikali kukupatia misaada, hao ni watu ambao hawawahurumii waliopatwa na matatizo hayo,” alisema Kamanda Kamugisha.
Tangu kutokea kwa maafa hayo, kumekuwa na mvutano baina ya wanasiasa na viongozi wa Serikali kuhusu utoaji wa chakula kwa waathirika, hali iliyosababisha baadhi yao kutoleana lugha chafu mbele ya wananchi.
Wakati huo huo, Benki ya NBC Tawi la Kahama imetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 5 kwa waathirika wa maafa hayo, yaliyotokana na mvua ya mawe iliyonyesha hivi karibuni katika Kijiji cha Mwakata wilayani hapa na kusababisha vifo vya watu 46.
Misaada hiyo ilikabidhiwa juzi na Meneja wa NBC Tawi la Kahama, Martin Nkanda ambaye alisema NBC inaungana na wasamaria wema waliojitolea misaada mbalimbali kwa waathirika wa maafa hayo.

Benki hiyo imekabidhi unga wa sembe mifuko 100, kilo 200 za maharage, ndoo 50 za mafuta ya kula yenye ujazo wa lita kumi kumi, chumvi, katoni 15 za sabuni za kufulia, shuka 100, mablanketi 100 na katoni 15 za madaftari kwa ajili ya wanafunzi walioathiriwa vifaa vyao vya masomo.

No comments:

Post a Comment