Kisima
kilichopo eneo la Matamwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambamo raia wawili
wa Ufaransa wanasadikiwa kuuawa na kisha kufukiwa kwa zege. Picha na
Mwinyi Sadallah
Zanzibar.Raia
wawili wa Ufaransa wameuawa na kutumbukizwa katika kisima cha maji
kilichomo ndani ya uwanja wa nyumba yao na watu wasiojulikana katika
eneo la Shehia ya Matemwe Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza kuwa watu hao mtu na mkewe
waliuawa hivi karibuni.
DCI
Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari vikosi vya Zimamoto na
Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima hicho na kwamba katika
hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu wa kushoto wa mmoja wa
watu hao.
Alisema
uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Wafaransa hao waliingia nchini
kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba kwenye ufukwe wa mwambao wa
Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza kuishi eneo hilo.
DCI
Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia watu watatu wakazi wa
Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja anayeishi katika eneo la
Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.
“Kuna
askari wanaendelea na kazi ya kuzamia ndani ya kisima kilichomo ndani
ya uzio wa nyumba hiyo, kazi bado ni kubwa na siyo ya siku moja,”
alisema DCI Ilembo.
Gazeti
hili limefanikiwa kufika katika eneo la nyumba hiyo na kukuta askari
Polisi wanne wakilinda nyumba hiyo huku harufu kali ikitoka katika shimo
la kisima.
Hata hivyo, mlinzi wa nyumba hiyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na simu yake kila ikipigwa imezimwa.
Mlinzi
mpya aitwaye Omar Juma ambaye amekutwa akilinda nyumba hiyo baada ya
kuajiriwa na mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa amesema alikabidhiwa kazi ya
ulinzi kuanzia Januari mwaka huu na hakumkuta mtu yeyote akiishi hapo.
“Kazi
yangu ni kazi za ulinzi, nimeletwa hapa na mwajiri, sijui lolote,
mwajiri wangu ndiye anayejua kama kulikuwa na watu kabla au la, sina la
kusema na sijui nianzie wapi,” alisema Omar.
Sheha wa Matemwe Kusini
Sheha
wa Shehia ya Matemwe Kusini, Denge Khamis Silima aliyelizungumzia suala
hilo kwa niaba ya Sheha wa Matemwe Kaskazini, aliliambia gazeti hili
kuwa taarifa za kutoweka kwa wazungu hao zilianza kuenea kuanzia Desemba
27 mwaka jana.
Denge
alisema alianza kupata taarifa za awali kutoka kwa mjumbe mmoja wa
Shehia aitwaye Mkadam Tabu Vuia kwamba mlango wa nyumba ya wazungu hao
ulikuwa wazi kwa muda mrefu na harufu kali ikitoka na inzi wakubwa
wametanda katika eneo hilo.
“Nimeshiriki
katika kazi ya kuchimbua kisima, askari wametoa mfupa wa mguu na unyayo
unaoaminika kuwa ni wa mtu, ingawa tuliikuta nyumba ikiwa haikuvunjwa
milango,” alisema.
Alisema
waliingia ndani ya nyumba hiyo kupitia dirishani wakakuta mbwa wa
wazungu hao, Allan naye amekufa na kwamba kwa sasa wanasubiri ripoti ya
uchunguzi wa polisi.
Sheha
huyo wa Shehia ya Matemwe Kusini alisema mazingira waliyoyakuta ndani
ya nyumba hiyo yameonyesha kuwa haikuhamwa kwa muda mrefu na kama kwamba
wanatarajia kurejea wakati wowote.
Alisema
baada ya kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, askari polisi
walifika katika eneo hilo na kazi ya kuchimba kisima ilianza baada ya
kubaini harufu kali ilikuwa inatoka kisimani.
Hata
hivyo, kazi ya kuchimba kisima ilikuwa ngumu baada ya kukutana na zege
lililojazwa na walipoendelea kuliondoa zege hilo walipata mguu mmoja wa
binadamu.
Denge
alisema zoezi la uchimbaji wa kisima hicho lilikwama juzi kutokana na
ugumu wa zege na hivyo kazi hiyo kuahirishwa na kuendelea jana baada ya
kupatikana mashine ya kuchimbua vitu vigumu na vifaa ya kuongeza hewa ya
oksijeni.
“Bado
hatujafanikiwa kubomoa zege na kuingia kina kirefu kujua kama ipo
mifupa zaidi au la, tunawasubiri polisi na askari wa zimamoto waje na
vifaa,” alisema Denge.
Agosti 7, mwaka jana raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali mjini Zanzibar.
Tukio
hilo lilitokea saa 1:15 usiku Mtaa wa Shangani eneo la Mji Mkongwe wa
Zanzibar, karibu na ofisi za Serikali ikiwamo Wizara ya Sheria na Wizara
ya Katiba na Maendeleo ya Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto.
Wasichana hao walifika Zanzibar kwa mwaliko wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Arts in Tanzania.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment