Pages

Thursday, October 27, 2011

MAMA KIKWETE KUONGOZA MATEMBEZI YA HIYARI KUSAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI


(Bebi Kapenya- MAELEZO)
Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, anatarajia kuzindua matembezi ya hiyari ya kuchangisha fedha kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuwasaidia watoto 527 wenye mahitaji maalumu waishio mikoa sita ya Tanzania. Watoto hao ni wale wanaosumbuliwa na magonjwa ya Kansa na Virusi vya UKIMWI waliolazwa katika wadi maalum katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edge Entertainment Bw. Edwin Ngere alisema, matembezi hayo yamedhaminiwa na kampuni yake ikishirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la ‘Children in Crossfire’ na yataanzia katika viwanja vya Mashujaa, Mnazi Mmoja na kuishia katika hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam tarehe 5 Novemba, 2011.
Bw. Ngere alisema kuwa, watu wanaweza kutoa michango yao kama vile magodoro, maji ya kunywa, nguo, maziwa ya unga, mafuta ya kupikia pamoja na nauli kwa ajili ya kurudi makwao.
Bw. Ngere aliongeza kuwa, yeyote anayetaka kushiriki itambidi kununua kadi zinazouzwa kwa shilingi elfu kumi kwa watu wazima na elfu tano kwa watoto.
Alisisitiza kwamba, kadi hizo zinapatikana katika vituo vya Ubungo Plaza, Clouds FM, SamakiSamaki Mlimani City, Shoppers Plaza, Kituo cha mafuta cha Big Born cha Kariakoo na Sinza na Shear Illusion Saloon.
Naye Balozi wa Uzazi Salama ndani na nje ya Tanzania, Bi. Stara Thomas aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili kusaidia watoto hao ambao wanahitaji uangalizi mkubwa kutoka kwa jamii nzima ya Watanzania.
Mradi huo unaoitwa ‘SAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI’ umeanza kutekeleza majukumu yake katika mikoa sita tu ya Tanzania ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro na kwamba mradi huu ni endelevu.

No comments:

Post a Comment