Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, October 24, 2011

RAMADHANI NDIYE MCHEZAJI BORA WA SEPTEMBA YASEMA TFF


Kiungo wa timu ya Coastal Union, Sabri Ramadhan ‘China’ amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba katika Ligi Kuu ya Vodacom.

China alichaguliwa kutokana na kupata pointi nyingi kwenye mechi alizocheza kwa mwezi huo. Baadhi ya mechi alizopata pointi nyingi ni dhidi ya African Lyon na JKT Ruvu Stars.

Katika mechi namba 27 dhidi ya Lyon iliyochezwa Septemba Mosi kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam na timu yake kushinda bao 1-0 alipata pointi 85 kati ya 100.

Vilevile alipata pointi 89 kwenye mechi namba 33 dhidi ya JKT Ruvu Stars iliyochezwa Septemba 5 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam. Coastal Union ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0.

Kwa kuibuka mchezaji bora wa Septemba, China atazawadiwa kitita cha sh. 600,000 kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom

Mchezaji bora wa Agosti alikuwa kiungo wa Polisi Dodoma, Ibrahim Massawe ambaye kwenye mechi namba 4 ya ligi hiyo dhidi ya African Lyon iliyochezwa Agosti 20 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma alipata pointi 93 ambazo hazikufikiwa na mchezaji yeyote kwa Agosti.

MCHEZAJI AOMBEWA ITC POLAND
Chama cha Mpira wa Miguu Poland (PZPN) kimetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Khatib Waziri Mzee ili aweze kucheza mpira wa miguu nchini humo.

PZPN imetuma maombi hayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kumwezesha mchezaji huyo kuichezea timu ya LUKS Wierzbiecice ambayo hata hivyo haikuelezwa iko ligi ya daraja gani nchini humo.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa PZPN, Zdzislaw Krecina, Mtanzania huyo aliyezaliwa Julai 30, 1974 ameombewa hati hiyo kama mchezaji wa ridhaa kwa maelezo kuwa hakuwahi kusajiliwa na klabu yoyote nchini.

TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika.

LIGI KUU YA VODACOM
Mechi za wiki hii za Ligi Kuu ya Vodacom ni kama ifuatavyo;

Oktoba 24- Coastal Union vs Polisi Dodoma (Uwanja wa Mkwakwani)
Oktoba 24- African Lyon vs Villa Squad (Uwanja wa Chamazi)
Oktoba 25- Moro United vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Chamazi)
Oktoba 25- Mtibwa Sugar vs Azam (Uwanja wa Manungu)
Oktoba 26- Toto Africans vs Kagera Sugar (Uwanja wa CCM Kirumba)
Oktoba 28- JKT Ruvu vs African Lyon (Uwanja wa Chamazi)
Oktoba 29- Yanga vs Simba (Uwanja wa Taifa)
Oktoba 29- Polisi Dodoma vs Oljoro (Uwanja wa Jamhuri)
Oktoba 29- Toto Africans vs Coastal Union (Uwanja wa CCM Kirumba)
Oktoba 30- Kagera Sugar vs Azam (Uwanja wa Kaitaba)
Oktoba 30- Villa Squad vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Chamazi)
Oktoba 30- Mtibwa Sugar vs Moro United (Uwanja wa Manungu)

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Oktoba 24 mwaka huu)
Muda: Saa 6.00
Mahali: TFF

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment