Pages

Monday, October 31, 2011

TAIFA STARS YAPANGIWA MSUMBIJI CAN 2013

TAIFA STARS YAPANGIWA MSUMBIJI CAN 2013



Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kucheza na Msumbiji katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2013 nchini Afrika Kusini.
Upangaji ratiba wa mechi hizo za mchujo ulifanywa juzi (Oktoba 28 mwaka huu) na kamati ndogo ya michuano hiyo mjini Malabo, Equatorial Guinea.
Jumla ya nchi 47 ikiwemo mwenyeji Afrika Kusini ndizo zilizothibitisha kucheza michuano hiyo. Nchi 16 zilizofuzu kucheza fainali za mwakani nchini Gabon na Equatorial Guinea zenyewe zimepitishwa moja kwa moja hadi raundi ya mwisho ya mchujo itakayoanza baada ya fainali za 2012.
Raundi ya kwanza ya awali itahusisha nchi nne ambazo kwenye ubora wa viwango ndizo ziko chini ili kupata mbili zitakazoingia raundi ya pili ya awali itakayokuwa na nchi 28. Nchi hizo ni Swaziland, Sao Tome, Lesotho na Shelisheli.
Stars imepangiwa kucheza na Msumbiji katika raundi hiyo ya pili ya awali. Tarehe za mechi hizo ambazo zitachezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2012 zitatangazwa baadaye.
Mechi nyingine za raundi hiyo zitakuwa kati ya Ethiopia na Benin, Rwanda na Nigeria, Congo na Uganda, Burundi na Zimbabwe, Algeria na Gambia, Kenya na Togo, Sierra Leone na mshindi kati ya Sao Tome na Lesotho.
Nyingine ni Guinea Bissau na Cameroon, Chad na Malawi, mshindi kati ya Shelisheli na Swaziland dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Misri, Madagascar na Cape Verde na Liberia na Namibia.
Timu 14 zitakazopita hatua hiyo zitaungana na 16 zilizofuzu kwa ajili ya fainali za Gabon/Equatorial Guinea kucheza raundi ya mwisho kupata 15 zitakazoungana na wenyeji Afrika Kusini kwa ajili ya fainali za 2013. Raundi hiyo itachezwa kati ya Septemba na Oktoba mwakani

No comments:

Post a Comment