WANAWAKE WATAKIWA KUTUMIA NAFASI WANAZOPEWA NA UNIFEM
Na Anna Nkinda- Perth Australia
30/10/2011 Wanawake wametakiwa kutumia nafasi zinazotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wanawake (UNIFEM) katika
kujiletea maendeleo yao na ya mataifa yao kwani lengo kuu la
kuanzishwa kwa shirika hilo ni kumuinua mwanamke na kuleta usawa wa
kijinsia.
Hayo
yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dk. Noeleen
Heyzer wakati akiongea na wake wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya
Madola katika mkutano wao uliofanyika Perth nchini Australia.
Dk. Heyzer alisema kuwa hivi sasa katika nchi nyingi Duniani wanawake wanapewa nafasi za kupata elimu, kuwezeshwa kiuchumi, usawa wa kijinsia , kupata afya bora kwa mama na mtoto na upatikanaji wa ajira hii yote ni kumfanya mwanamke aweze kujiinua kiuchumi kwani hapo zamani wanawake walikuwa wameachwa nyuma kimaendeleo tofauti na wanaume.
“UNIFEM
inashughulika na masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake
kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo basi ni jukumu lenu kuwahamasisha
wanawake katika nchi mnazotoka ili waweze kuzitumia nafasi wanazopewa
hii itawasaidia kujikwamua kiuchumi”, alisema
Baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNIFEM kumaliza kuongea na wake hao wa wakuu wan chi akiwemo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete walitembelea Halmashauri ya jiji la
Perth upande wa Sekta ya Nishati na Madini na kuelezwa jinsi sekta hiyo
ilivyochangia kutoa ajira na kuinua uchumi wa nchi hiyo.
Viongozi
kutoka makampuni ya uchimbaji wa madini ambao ni Mtendaji Mkuu wa
Chamber of Minerals and Energy of West Australia Reg Howard-Smith,
Mkurugenzi Mtendaji wa Argyle Diamonds Kevin McLeish na
Josephine Archer ambaye ni meneja biashara kutoka Argyle Pink Diamonds
walisema kuwa kutokana na jiografia nzuri mji huo umejaliwa kuwa na
madini mengi ukilinganisha na miji mingine.
“Upande
wa Magharibi wa Nchi yetu kuna miji minne ambayo ni Kimberley,
Pilbara, Yilgarn na Kusini Magharibi ambako kunapatikana madini zaidi
ya aina 50 baadhi yakiwa ni dhahabu,
almasi, chuma, mchanga mzito wenye madini aina tofauti, base metals,
chumvi, chuma cha pua, Ilmenite, Rutile, Alumina, Zircon, Garnet na
Tantaluma”, walisema.
Wake
wa wakuu wan chi wanachama wa Jumuia ya madola waliweza kujionea aina
mbalimbali za madini yanayopatikana katika nchi hiyo pamoja na vito vya
thamani na bidhaa zinazotengenezwa kutokana na madini hayo.
Aidha
waliweza kutembelea bustani ya kutunza mimea na wanyama wa asili
nakuona jinsi viumbe hai vya kale vinavyotunzwa ili visiweze kupotea kwa ajili ya kumbukumbu ya vizazi vijavyo na wageni wanaotembelea nchi hiyo.
Mkutano wa wakuu wa Nchi wanachama ya Jumuia ya madola umemalizika leo na Kaulimbiu ya mwaka 2011 ya Jumuia hiyo ni “Wanawake ni wakala wa mabadiliko”
No comments:
Post a Comment