Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, November 3, 2011

BREAKINGNEWS......WAISLAMU MWANZA WAPIGWA MABOMU NA FFU


KWA mara nyingine tena, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, limelazimika kutumia nguvu kubwa kwa kufyatua mabomu ya machozi na risasi za moto hewani, kutokana na vurugu kubwa zilizotokea dhidi ya waumini wa dini ya Kiislamu, waliokuwa wamevamia kwenye Mahakama ya Mwanzo jijini hapa kisha kusababbisha taharuki kubwa.

Mwandishi wa mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kutoka mkoani mwanza Sitta Tumma anaripoti kuwa Vurugu hizo kubwa zilitokea leo majira ya saa 2:20 hivi asubuhi, baada ya waumini wa dini hiyo ya Kiislamu kuvamia katika Mahakama hiyo kwa lengo la kusikiliza kesi inayowakabili waumini wanne wa dini ya Kikiristu, ambao wanatuhumiwa kuchoma Korani, na baada ya mahakama kuwaachia kwa dhamana watuhumiwa hao, ndipo kasheshe ilipoanzia na kusababisha ghasia kubwa.

Kufuatia hali hiyo, waumini wengi wa Kiislamu walionekana dhahiri kupinga kitendo cha mahakama hiyo kuwapa dhamana watuhumiwa hao, licha ya sheria za nchi kuruhusu dhamana kwa kila raia kutegemea na kosa la mshakiwa.

Wakiwa wametanda nje ya mahakama hiyo, baadhi ya waumini hao wa dini hiyo ya Kiislamu, walisikika wakilalamikia kwa kusema kwamba, iwapo washakiwa hao watapewa dhamana na mahakama, wao wapo tayari kuwahukumu papo hapo, jambo lililoonekana kuwashtua watu wengi waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

"Tutatoa hukumu yetu hapa kama mahakama itawaachia watu hawa. Hatutaki pia kesi hii iendelee kuahirishwa mara kwa mara, tunataka haki itendeke vinginevyo tutawahukumu hapahapa, maana walichana Korani tukufu", alisikika muumini mmoja wa Kiislamu akisema nje ya mahakama hiyo.

Kufuatia hali hiyo, polisi walipata taarifa ya kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani katika eneo hilo la mahakama, na walifika haraka katika eneo hilo na kuwataka waumini hao kuondoka haraka kwenye eneo hilo, lakini walikataa kutii amri hiyo ya polisi.

Baada ya waumini hao kugoma kuondoka, polisi walilazimika kujipanga kisha kuanza kupiga mabomu ya machozi hewani, hali ambayo ilizua mtafaruku mkubwa, ambapo waumini hao wa Kiislamu walionekana kujibu mapigo kwa kuwashambulia polisi kwa mawe.

Polisi walipoona wanashambuliwa, walilazimika kujihami kwa kuzidisha mashambulizi kwa kufyatua mabomu ya machozi ovyo hewani, huku milio ya risasi za moto ikisikika, na kwamba baadhi ya barabara zilifungwa na kuzuiwa magari, pikipiki kuingia katikati ya jiji.

Katika vurugu hizo baadhi ya wananchi walijeruhiwa na mabomu hayo, ambapo Tanzania Daima ilishuhudia muuza magazeti mwanamke anayeuza magazeti katika eneo la Bantu akiwa amejeruhiwa shingoni na mkononi baada ya bomu la machozi kulipuka mbele yake.

Watu waliokuwa wakiingia katikati ya jiji, wakiwemo wafanyakazi walilazimika kushuka kwenye magari umbali wa zaidi ya kilometa tano, kisha kutembea kwa miguu hadi mjini, na kwamba askari polisi kitengo cha Usalama barabarani ndiyo waliokuwa wakiwajibika kuzuia magari yote yasiingie mjini kwa takriban saa mbili hivi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), alisema polisi walilazimika kutumia nguvu hiyo kubwa kwa lengo la kuimarisha usalama wa raia na mali zao, ikiwa ni pamoja na kuwatawanya waumini hao wa Kiislamu wasiendelee kufanya fujo mahakamani hapo.

Alisema, tayari kuna watu 19 wakiwemo baadhi ya viongozi wa Kiislamu wamekamatwa, na wanafanyiwa mahojiano maallumu na jeshi hilo la polisi, na kwamba jeshi hilo linawasaka watu wengine wanaodaiwa kusababisha vurugu hizo kubwa.

"Polisi hatuwezi hata siku moja kuruhusu uvunjifu wa amani utokee mahala popote. Na ndiyo maana tumelazimika kutumia nguvu kwa ajili ya kurejesha usalama!. Lakini tayari kuna watu 19 tumewakamata, na wamo baadhi ya viongozi wao...sheria lazima ifuate mkondo wake katika hili", alisema Kamanda Barlow.

Hivi karibuni waumini wa dini ya Kikiristu walifikishwa katika mahakama ya Mwanzo jijini Mwanza, wakituhumiwa kuchoma Korani tukufu, baada ya mwanamke mmoja muumini wa dini ya Kiislamu kuombewa na kubahatika kupata mtoto katika Kanisa moja jijini hapa na waumini hao kuamua kuchoma moto Korani hiyo kinyume cha sheria za nchi.

Miezi mitano iliyopita, Jeshi la polisi mkoani Mwanza, liliingia kwenye majaribu baada ya kulazimika kutumia mabomu na risasi za moto kupambana na ghasia kubwa zilizofanywa na wafanyabiashara wadogo jijini hapa , maarufu kwa jina la 'Machinga', ambapo waligoma kuondoka eneo la Makoroboi ambalo haliruhusiwi kuendesha biashara za machinga, kwani lipo karibu sana na msikiti na shule moja ya awali.

Mapigano hayo makali yaliyosababisha mtu mmoja kufariki dunia kutokana na kile kilichoelezwa kupigwa risasi ya aina ya Shortgun, ilikuwa ni mwendelezo wa vurugu kama hizo zilizowahi kufanyika tena kabla ya mwezi Juni mwaka huu, kisha kuleta kizaazaa kikubwa na kusababisha hasara kubwa.

No comments:

Post a Comment