Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, November 8, 2011

Serikali yatoa tamko kuhusu mikesha ya CHADEMA mkoani Arusha

Serikali yatoa tamko kuhusu mikesha ya CHADEMA mkoani Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa S. Mulongo
Wakati jeshi la Polisi mkoani Arusha likiwa limefanikiwa kuwasambaratisha wafuasi wa CHADEMA, ambao walikuwa wamejikusanya katika viwanja vya NMC, jijini hapo kwa lengo la kufanya mikesha ya amani, serikali mkoani humo, imetoa tamko zito kuhusu vurugu za kisiasa zinazoendelea kushamiri mkoani humo na hivyo kuhatarisha ustawi wa shughuli za kiuchumi.
Mwanzoni mwa wiki hii, maelfu ya wafuasi wa CHADEMA, walikusanyana katika viwanja vya NMC, maarufu kama Unga Limited, jijini Arusha, katika mkutano wa hadhara ambao chama hicho kupitia kwa katibu mkuu wake, kilitoa tamko la kufanya mikesha ya amani mahali hapo kwa lengo la kuishinikiza mahakama kumuachia huru mbunge wa jimbo la Arusha, Godbless Lema, ambaye anashikiliwa rumande kwa kukataa dhamana, katika kesi inayomkabili yeye na wafuasi wengine 18 wa CHADEMA.
Hatua hiyo, ililikwaza jeshi la Polisi ambalo liliingilia kati na kuwasambaza wafuasi hao wa CHADEMA, katika zoezi ambalo lilifanyika alfajiri ya jumanne, huku katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa na mbunge mwingine wa chama hicho, Tundu Lissu, wakikamatwa na Polisi, katika tukio ambalo inaelezwa kuwa mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, alifanikiwa kukimbia eneo la tukio kabla ya kukamatwa.
Viongozi hao pamoja na wanachama wengine 20, walifikishwa mahakamani mchana wa leo ambako walisomewa mashtaka ya kufanya mkusanyiko bila kibali, ambapo baadae Dk. Slaa na Lissu, waliachiwa kwa dhamana sanjari na wafuasi wengine 9, huku wengine 11 wakibakia rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Akizungumza na Jukwaa Huru, kwa njia ya simu jioni ya leo, mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa S. Mulongo, amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani mwake lilifanikiwa kusambaratisha wafuasi hao wa CHADEMA, bila kusababisha majeruhi kwa mtu yeyote yule, na akalipongeza jeshi kwa ufanisi na busara walizozitumia katika kufanikisha zoezi hilo.
“Zoezi la kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA, lilifanywa kwa utulivu mkubwa sana, na zaidi ya mabomu ya machozi, hakukuwa na matumizi ya silaha zingine za moto wala hakukuwa na wananchi wowote waliojeruhiwa katika tukio hilo na hivi tunavyoongea hali iko shwari huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kama kawaida” alisema mkuu wa mkoa.
Mkuu huyo wa mkoa amemuambia mwandishi wa Jukwaa Huru kwa njia ya simu kuwa, serikali imesikitishwa na kauli za kuchochea vurugu ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa CHADEMA, na kwamba serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa inadhibiti vitendo vya namna hiyo kwani licha ya kwamba havijayumbisha shughuli za kawaida za mji wa Arusha, zinatishia kudumaza maendeleo kama zikiachwa ziendelee.
“Ukweli ni kwamba hakujawa na athari zinazoweza kuelezwa kuwa zimefanya shughuli fulani za kawaida kudorora kwasababu wananchi walio wengi wangali wanaendelea na shughuli zao. Hata takwimu kuhusu utalii na hususan kwa miezi hii, hazionyeshi kuwa kuna anguko lolote la idadi ya watalii, lakini hatuwezi kuacha hali hii kuendelea;
“Wananchi na hata wafuasi wengine wa CHADEMA, tunapoongea nao wanaeleza wazi wazi kuwa wamechoshwa na hali hii na mimi kama msemaji wa serikali katika mkoa huu, nitoa wito kwa vyama vyote vya siasa kuachana na hizi siasa zinazoanza kushamiri za kiuchochezi na kishabiki zaidi, ni lazima ifike mahali viongozi hawa wajue kuwa wanatakiwa kuwatumikia wananchi na hatuwezi kuleta maendeleo kwa mikusanyiko ya kila siku namna hii” alifafanua Bw. Magesa.
Amesema kuwa, serikali imeanza kuchukua hatua za kuona hali mjini Arusha na katika mkoa huo kwa ujumla unarejea katika hali ya amani ambapo tayari yeye kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameshaanza kufanya vikao vya kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa hali ya amani na uelewano baina ya wanasiasa unarejea na kuurejesha mkoa wake katika hali tulivu
“Tunataka kuanza upya, hatuwezi kuendelea kuangalia siasa hizi ambazo zinatishia ustawi wa kimaendeleo ziendelee kukua mkoani hapa. Tumeanza kukutana na wadau mbalimbali na hususan viongozi wa kidini na tutaendelea kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa wa vyama mbalimbali kwa lengo la kuona ni njia gani iliyo sahihi na bora ya kuendesha shughuli za kisiasa kwa lengo la kukuza maendeleo ya mkoa na sio kusimamisha kazi za uzalishaji kila kukicha kwa mikusanyiko isiyo na tija” aliongeza.
Endelea kufuatilia habari zetu, ambapo tutakuletea mahojiano hayo moja kwa moja kama yalivyofanywa na mwandishi wetu kwa njia ya simu.

No comments:

Post a Comment