Pages

Friday, November 11, 2011

Udhamini ligi ya Zanzibar mashakani

Udhamini ligi ya Zanzibar mashakani

ZFA
Ligi ya Zanzibar mashakani
Udhamini wa ligi kuu ya soka ya Zanzibar uliokuwa ufanywe na kampuni ya usafiri wa baharini ya Seagull umeingia wasiwasi baada ya hatua ya serikali kuisimamisha meli hiyo ya abiria.
Ligi kuu ya Zanzibar iliyokuwa ianze mwezi agosti ilichelewa kwa kukosa wadhamini na ilipoanza wiki iliyopita ikapigwa stop kwa sababu ya shauri la timu ya malindi katika mahakama ya Zanzibar.
Sasa Malindi wamefuta kesi yao baada ya kununua daraja kwa kuichukua timu ya Miembeni United na chama cha soka kilikuwa kimepanga ligi hiyo ianze rasmi siku ya Ijumaa.
Lakini vilabu vikijipanga imedhihirika kuwa dau la mnyonge haliendi joshi pale serikali ilipoilima barua kampuni ya Seagull iliyojitwisha jukumu la kudhamini ligi hiyo kwa mamlaka za usafiri wa bahari kuisimamisha meli ya Seagull.
Serikali imesema kwa sababu za kiusalama meli hiyo inasimamishwa kwa muda usiojulikana na kampuni hiyo tayari imeshaiarifu ZFA juu ya hali hiyo ambapo inaelekea udhamini utaota mbawa.
Katibu mkuu wa ZFA Mzee Zam alithibitisha hali hiyo na kusema imewavunja moyo ingawa alikiri kuukubali uamuzi wa serikali kwa kuzingatia hadhari inayochukuliwa kutokana na ajali ya MV Spice Islander ya septemba 10 iliyouwa mamia ya abiria.
Kwa hivyo ligi itakua ya pangu pakavu na Mwandishi wa BBC Zanzibar, Ally Saleh anasema hali hiyo itaziwia vigumu timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo kwa ukosefu wa fedha za kujikimu.
Udhamini huo ulikuwa ugharimu Tanzania shilingi milioni 75 ulipokewa vyema na vilabu kwa vile iliaminika ingeifanya ligi hiyo kuwa na ushindani.
Mara ya mwisho Ligi ya Zanzibar kupata udhamini ilikuwa ni kupitia kampuni ya simu za mkononi ya ZANTEL kwa misimu ya 2006/2007 na 2007/2008.

No comments:

Post a Comment