Pages

Sunday, November 6, 2011

WAZAZI ACHENI KUSEMA UONGO - PINDA

WAZAZI ACHENI KUSEMA UONGO - PINDA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wazazi wenye uwezo wa kulipia watoto wao katika Vyuo Vikuu waache kusema uongo kwani kwa kufanya hivyo wanawakosesha watoto wa maskini kupata mikopo wanayostahili.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Novemba 5, 2011) wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya pili ya Chuo Kikuu cha St. John’s yaliyofanyika kwenye chuo hicho mjini Dodoma. Jumla ya wahitimu 1,002 walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada na stashahada za juu katika fani za theolojia, uuguzi, famasia, sayansi na ualimu, biashara, uhasibu na fedha, masoko na teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Bado kuna malalamiko nayapata kupitia njia mbalimbali kuhusu utaratibu wa Bodi ya Mikopo hasa pale watoto wa maskini, tena waliofaulu vizuri wanapokosa mikopo. Nawasihi wazazi wenye uwezo waache kusema uongo kwa sababu si busara kuwatumia watoto wao kupata mikopo wakati watoto wanaostahili wanaikosa…,” alisema.
Alisema wazazi wakiwa wakweli na kuamua kuwalipia watoto wao, fursa za watoto maskini kupata mikopo zitaongezeka.
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia changamoto zinazoikabili Serikali katika kukabiliana na kasi ya ongezeko la watu na kuonya kuwa linaleta changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za jamii.
“Ongezeko la watu liko juu sana na kasi yake haioani na ukuaji wa uchumi… ukuaji huu unaathiri sana nyanja nyingi hasa elimu na ndiyo maana tunakabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaoomba mikopo katika Bodi ya Mikopo kila mwaka,” alisema.
Alikitaka Chuo Kikuu kikuu cha St. John’s kiweke mikakati maalumu ya kusomesha wanataaluma wake wenyewe kwa sababu utaratibu wa kuazima wanataaluma kwa njia moja au nyingine unawakwaza wanafunzi kwani hawapati muda wa kutosha wa kuwasiliana na mwalimu wao.
”Nawasihi muongeze bidii ya kusomesha wanataaluma wenu kwa kasi ile ile ya kuongeza wanafunzi katika vyuo vyenu. Kama Taasisi inayojitegemea hamna budi kusomesha wataalam wenu wenyewe kwa msaada wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,” alifafanua.
Akitoa wosia kwa wahitimu, Waziri Mkuu alisema: “Ombi langu kwenu ni kuwa, mkatumie elimu mliyoipata hapa chuoni kwa manufaa yenu, jamii na Taifa kwa ujumla. Msianze kwa kujifikiria nafsi zenu, kwani huo ni mwanzo wa tamaa, uchoyo, dhuluma, rushwa na pengine wizi.”

No comments:

Post a Comment