NAMFAHAMU
vyema na nimekuwa nikifuatilia nyendo zake kwa karibu mwanamuziki
nguli wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Charles Gabriel
Cyprian 'Chaz Baba' tangu alipotua bendi hiyo akitokea Mchinga Sound.
Wakati huo Mchinga Sound ilikuwa
ikimilikiwa na aliyepata kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na
Michezo na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na
Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mudhihir Mudhihir.
Uhamisho wa Chaz Baba kutoka Mchinga
Sounda kwenda Twanga Pepeta ulizua tafrani kubwa kati ya Mudhihir na
Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET),
Asha Baraka, hadi kufikia hatua ya kurushiana makonde Leaders Club.
Tuyaache hayo! Chaz Baba ambaye ni
mwimbaji, mtunzi na rapa, alizaliwa mwaka 1981 jijini Dar es Salaam.
Alipata elimu ya msingi na sekondari lakini aliishia kidato cha pili
mwaka 2004. Shughuli za muziki alianza tangu akiwa masomoni.
Alijiunga na bendi ya Jandaheka ya
Bagamoyo na baadaye Less Bandu. Baada ya bendi hizo mbili alijiunga na
Stone Musica 'Wajelajela Original'.
Baadaye akaenda Tanga kuanzisha bendi
iliyojulikana kwa jina la Fax Jazz. Mambo hayakuwa mazuri, akajiunga na
Sot Sound ya Dar es Salaam, baadaye akaenda Mchinga Sound ambako
hakukaa sana, akajiunga na Twanga Pepeta, ambayo jana alitangaza rasmi
kuachana nayo!
Ajiondoa Twanga
Wakati akitangaza kuiacha Twanga
Pepeta leo, Chaz Baba alidai sasa ameamua kuwa mwanamuziki huru wa
kujitegemea, na amejiondoa katika bendi hiyo kwa madai ya kukosa
mkataba kwa muda mrefu.
Chaz Baba anasema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa akili zake timamu kutokana na majukumu ya kifamilia aliyonayo.
Anasema alisaini mkataba wa mwaka
mmoja wakati anajiunga na Twanga Pepeta mwaka 2005, lakini baada ya
hapo alikuwa akipiga 'deiwaka' kwa kuitumikia bendi kwa mazoea bila ya
kuwa na mkataba.
Twanga yakana
Hata hivyo, Meneja wa Twanga Pepeta,
Hassan Rehani anasema Chaz Baba alisaini mkataba wa miaka mitano na
bendi hiyo hivi karibuni, pia akalipiwa na kodi ya nyumba sh. milioni
2.5, na kwa vile hajafuata taratibu za kuuvunja, watawasilishwa
malalamiko yao Mahakama ya Biashara kwa hatua za kisheria.
Rehani anasema wanajua kuna mipango ya
chini chini inaendeshwa kuidhoofisha Twanga Pepeta, lakini anabainisha
wanaofanya hivyo hawatafanikiwa, na bendi hiyo itazidi kusimama imara.
"Haiwezekani tangu mwaka 2005 Chaz
Baba hajapewa mkataba... madai kwamba alikuwa akifanya kazi kama
'Deiwaka' kwa takriban miaka sita si ya kweli... huku ni kukosa
fadhila, tena hakuna mwanamuziki aliyelelewa vyema kama Chaz Baba,"
anadokeza Rehani.
Bendi haitasambaratika
Rapa huyo aliyekuwa miongoni mwa
waimbaji mahiri wa bendi hiyo, inawezekana kuondoka kwake likawa pigo
kutokana na uhodari wake wa kuimba alipokuwa Twanga Pepeta.
Nyota huyo wa muziki wa dansi nchini
anasema anachofanya sasa ni kufanya kazi kwa mikataba na si vinginevyo,
hali ambayo itamsaidia kujua haki zake za msingi popote
atakapohitajika.
Hata hivyo, mmoja wa wanamuziki
wakongwe wa Twanga Pepeta anasema kuondoka kwa Chaz Baba si pengo
kubwa, isipokuwa watamkosa kutokana na mazoea waliyokyuwa nayo kwake.
"Kuondoka kwa Chaz Baba
hakutaisambaratisha Twanga Pepeta, isipkuwa mazoea tutamkosa kutokana
na mazoea, lakini hali itarejea kama kawaida kama ilivyokuwa kwa
Ramadhan Masanja 'Banza Stone', Ally Chocky na wengine.
"Hao wanaohangaika kuisambaratisha
Twanga Pepeta bado hawajajua kilipo chanzo cha mizizi na shina...
wanahangaika bure," anasema mwanamuziki huyo ambaye hakupenda kutajwa
jina gazetini.
Anatoa mfano kuwa hata Jumatano
iliyopita, Chaz Baba hakwenda kazini Billicanas, lakini mashabiki
hawakuhisi kuona pengo lake, kwa vile wanamuziki wengi waliopo wanamudu
kuimba sauti yake.
Ameahidiwa gari, mil 17/-
Meneja wa Chaz Baba, Bernard Msemwa,
anasema siku chache zijazo, mwimbaji huyo atakwenda nje ya nchi kwa
ajili ya mapumziko ya wiki moja ili ajipange upya katika tasnia hiyo ya
muziki wa dansi.
Msemwa anaongeza kuwa mwanamuziki huyo
yuko huru kujiunga na bendi yoyote ikiwemo Twanga ikiwa kutakuwepo na
mkataba tofauti na ilivyokuwa awali.
Hata hivyo, habari kutoka ndani kwa
wadau wa karibu na Chaz Baba zimedokeza kuwa msanii huyo ametangaza
kuwa mwanamuziki huru kutokana na mipango iliyosukwa na mmiliki wa
bendi ya Mashujaa, Hoseah Hopaje 'Maisha' ambaye ni Mhasibu Mkuu wa
Shirika la Ndege la Oman 'Oman Air' akishirikiana na Chocky wa Extra
Bongo.
Inadaiwa kuwa Maisha na mkewe, Mama
Sakina, ambao ni washirika wakubwa wa Mkurugenzi wa ASET inayomiliki
Twanga Pepeta, Asha Baraka, ndio wamesuka mipango ya kumng'oa Chaz Baba
kwenye bendi hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha anatua Mashujaa ili
kuuimarisha bendi hiyo, na ameahidiwa kupewa nafasi ya urais wa bendi.
"Maisha na Mama Sakina wametumia
mwanya huo kumuondoa Chaz Baba Twanga Pepeta ili aonekane ni
mwanamuziki huru, kisha muda mfupi ujao atatangaza kutua Extra Bongo
inayoongozwa na Chocky, na baadaye atahamia Mashujaa.
Kibosho, Kanuti watakiwa
"Chaz Baba amewapa masharti ya
kuondoka na baadhi ya wanamuziki Twanga Pepeta wakiwamo wapiga vyombo,
Godfrey Kanuti, Hassan Kado, James Kibosho na wanenguaji Asha Said
'Sharapova' na Betty Mwangosi 'Baby Tall'," anadokeza mpasha habari
ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Chanzo hicho cha habari kinadokeza
kuwa Chaz Baba ambaye Jumatano usiku hakujumuika na wenzake kazini
Billicanas, siku hiyo alikuwa Hoteli ya Holiday Inn ghorofa ya 10 akiwa
na Maisha na washirika wake, ambapo alipewa donge nono la sh. milioni
17 na ahadi ya gari aina ya Noah ambalo ndilo ataondoka wakati wowote
kuanzia wikiendi hii, kwenda Dubai kulichukua.
Maisha akana
Maisha ambaye awali alikuwa Mhasibu
Mkuu wa Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM), alipoulizwa kuhusu madai
hayo alikanusha na kusema kuwa hahusiki kwa lolote.
"Si kweli kwamba nimehusika na mipango
ya kumng'oa Chaz Baba Twanga Pepeta, ingawa Oktoba 2011 alinifuata
kunishawishi kwamba ajiunge Mashujaa, lakini nilimkatalia na
nikamwambia Asha Baraka habari hizo ili kama hana mkataba
wamuandalie... kama ningekuwa na mpango huo nisingemwambia Asha,
ningemchukua tangu wakati huo.
"Asha na kaka yake ambaye ni
Mwenyekiti wa ASET, Baraka Msiilwa tuliwasiliana nao mapema na
niliwaeleza habari za Chaz Baba... si kweli kwamba alikuwa akitakiwa
Mashujaa.
"Hata hivyo, bado ana nafasi ya kurudi Twanga Pepeta wakifikia makubaliano na akapewa mkataba na waajiri wake wa zamani.
"Lakini pia hata sisi Mashujaa kama
tunaweza kufikia makubaliano na Chaz Baba na ASET wakituruhusu,
tunaweza kumchukua," anasema Maisha.
Hata hivyo, mmoja wa mameneja wa
Twanga Pepeta, Martin Sospeter anasema mikataba ya wanamuziki wa bendi
hiyo haina budi kuheshimiwa, na anamshangaa Chaz Baba kwa kukosa
fadhila.
"Kuna wadau wa muziki wanaamini kuwa
bila kuibomoa Twanga Pepeta bendi zao haziwezi kusimama imara, ndiyo
maana wanahangaika usiku na mchana kuimaliza, lakini hawatafanikiwa
asilani," anasema Sospeter.
Sospeter anadokeza kuwa hata
wanamuziki wengine wanaotajwa kutaka kuondoka, Kibosho, Kanuti, Kado,
Sharapova na Baby Tall, wote wana mikataba isiyopungua miaka mitatu
kila mmoja, na anaamini kila mmoja ataheshimu hilo.
Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu
anasema wanamtakia kila la heri Chaz Baba huko aendako, lakini
akabainisha Twanga Pepeta ni chuo cha mafunzo ambacho waliondoka
wanamuziki wengi nguli wakiwamo 'Banza Stone, Chocky na wengine, lakini
kila kukicha inazidi kuimarika.
TRA Kushirikiana na Viongozi wa Serikali za Mitaa Kuimarisha Ukusanyaji
Kodi Kariakoo
-
Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi wa Kariakoo, Kabula Mwemezi (aliyesimama)
akizungumza katika wa semina ya siku moja kwa viongozi wa Serikali za mtaa
mkoa wa...
1 hour ago
No comments:
Post a Comment