Jeshi
la polisi mkoani Mbeya limeendelea kujisiriba matope kwa kuendesha
mauaji ya kiholela kwa raia ambapo jana askari wa jeshi hilo wamemuua
mwanafunzi Said Msabaha wa shule ya Sekondari Lupa iliyopo wilayani
Chunya mkoani hapa.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Lupa wilayani humo William Patrick Mbawala, ameuambia
mtandao wa huu kuwa mwanafunzi huyo kabla ya kifo chake alikamatwa na
askari hao akiwa na wenzake watatu kwa tuhuma za wizi wa simu Februari
29, mwaka huu na baadaye waliachiwa kwa dhamana.
Amesema
baada ya kutolewa katika kituo kidogo cha Lupa, Marehemu alionekana
kuwa hali yake imedhoofika na alipoulizwa alieleza kuwa alipokuwa
kituoni hapo alipigwa na askari polisi jambo ambalo liliwalazimu
kumpeleka katika zahanati ya kijiji hicho chini ya Mganga aliyemtaja kwa
jina la Dr. Solomon.
Amesema
Baada ya kuona hali yake inaendelea kuwa mbaya ndipo lilipochukuliwa
jukumu la kumpeleka Hospitali ya wilaya na bahati mbaya akafia njiani
hata kabla ya kumfikisha katika Hospitali hiyo.
Naye
Baba mzazi wa marehemu, Msabaha Hussein, amesema kuwa baada ya kufariki
mtoto wake akachukua jukumu la kupeleka maiti kituo cha polisi ili
wahusike katika kuuzika mwili wa marehemu kwa kile aichodai kuwa kifo
cha mwanae ni matokeo ya kipigo walichokitoa alipokuwa mikononi mwao.
Nao
baadhi ya wananchi waliohojiwa kwa masharti ya kuhifadhi majina yao
wamesema kuwa baada ya kuona hali hiyo na kwasababu askari wanaodaiwa
kuhusika wanawafahamu ndipo walipochukua jukumu la kuwatafuta askari hao
ambao tayari walikuwa wametokomea kusikojulikana.
Wamesema
kuwa baada ya kuwakosa katika makazi yao, waliamua kuzichoma moto
nyumba za askari hao ambao ni Copl. Maxmillian, PC Mjuni na PC Hery
ambapo hawakuishia hapo walimtafuta PC Fadhil bila mafanikio na kuharibu
samani zake za ndani huku wakishinikiza Jeshi la polisi kuuzika mwili
wa marehemu huyo.
Afisa upepelezi wa Jeshi hilo mkoani Mbeya (RCO) Elias Mwita alipotakiwa kuzungumzia sakata hilo alisema kuwa ni mapema mno.
Mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Chunya Deodatus Kinawiro ambaye
ni Mkuu wa wilaya hiyo alipotafutwa ili aweze kuzungumzia tukio hilo
hajaweza kupatikana kupitia simu yake ya kiganjani.
Awali
askari hao walidaiwa kutorokea Jijini Mbeya lakini taarifa kutoka ndani
ya vyanzo vya kikosi kazi cha mtandao huu jeshi la Polisi mkoani Mbeya
vimesema kuwa askari hao walikuwa bado hawajakamatwa wala kuonekana
katika viunga vya Jiji la Mbeya.
Tukio
hilo la kinyama limetokea siku chache baada ya askari wa jeshi hilo PC
Maduhu kuhusika kumuua aliyekuwa Mwanafunzi wa chuo kikuu cha TEKU
kilichopo jijini mbeya Daniel Godluck Mwakyusa (31) February 14, mwaka
huu.
Habari na Ezekiel Kamanga, Chunya.
|
No comments:
Post a Comment