Pages

Sunday, April 29, 2012

CHEKA APATA AJALI NA GARI YAKE ALIYOSHINDA JANA USIKU



 Gari la Cheka likiwa Kituoa cha Polisi Magomeni baada ya kupata ajali jana usiku.
***************************
*Furaha ya ushindi wa Cheka kumchapa maugo yaishia kituo cha Polisi
*Alala Oysterbay Polisi adhaminiwa leo
 BAADA ya Bondia mahiri  Francis Cheka kuibuka na ushindi mnono wa TKO dhidi ya mpinzani wake Mada maugo na kukabidhiwa mkanda wa ubingwa wa Afrika Mashariki IBF na Gari lenye thamani ya Sh. Milioni 8, katika pambano lao lililofanyika jana usiku katika Ukumbi wa PTA, furaha ya bondia huyo iliishia mikononi mwa Polisi.

Ikiwa ni siku moja tu baada ya kuvishwa taji la ubingwa huo na kukabidhiwa mchuma wake, Cheka alikamatwa na Polisi masaa machache tu baada ya kukabidhiwa gari na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwake ambayo iliishia mitaa ya Manzese baada ya kupata ajali kwa kugonga Pikipiki na kuwajeruhi dereva wa pikipiki hiyo na abiria wake ambao walikimbizwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.

Pikipiki iliyogongana na gari la Cheka
Leo asubuhi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo mtandao huu wawww.sufianimafoto.blogspot.com, ulifanya jitihada za kupata dondoo za tukio hilo na kufika Kituo cha Polisi Oysterbay ambako alikuwa ameshikiliwa Bondia huyo na kupata taarifa kuwa muda mchache tu uliopita kabla ya kuwasili mahala hapo aliondoka akiwa ameongozana na nduguze baada ya kupata dhamana.

Baada ya kupishana na bondia huyo mtandao ulitinga Kituo cha Polisi Magomeni na kufanikiwa kuliona gari hilo likiwa limeharibika na kuvunjika kioo huku Pikipiki hiyo iliyogongwa yenye namba za usajiri T507 BYR, ikiwa mahala hapo.

Akizungumza na Mtandao huu kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokea jana usiku majira ya saa nane maeneo ya Manzese na kuwajeruhi dereva na abiria wake waliokuwa katika pikipiki hiyo.

Aidha Kenyela, alisema kuwa baada ya ajali hiyo Dereva wa gari hilo lenye namba za usajiri T 321 AAU, aliyefahamika kwa jina la Francis Cheka, alifikishwa kituo cha Polisi Oysterbay na kushikiliwa hadi asubuhi ya leo walipofika ndugu zake na kumuwekea dhamana.

Akielezea tukio hilo Kenyela, alisema kuwa Gari la Cheka lilikuwa likitokea maeneo ya Manzese kuelekea Ubungo na Pikipiki ikitokea Ubungo kuelekea Manzese na walipofika maeneo ya Tip Top Manzese, dereva wa pikipiki aliutan na kuhamia barabara ya pili ili kuelekea Ubungo na kugongana na gari hilo.

Aidha alisema kuwa dereva huyo wa pikipiki bado amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala akiendelea na matibabu huku abiria wake akitibiwa usiku wa jana na kuruhusiwa.

 Kenyela aliwataka madereva wa pikipiki kufuata na kuheshimu sheria za usalama Barabarani ili kuepuka ajali za kizembe za kila siku zinazokatisha maisha yao.

No comments:

Post a Comment