Na Luqman Maloto
Wiki
iliyopita tulianza kujadili mada ya wivu na dawa zake. Tuliangalia
mbinu muhimu zinazoweza kukufanya ukaondokana na tatizo la wivu wa
kupitiliza kwa mwenzi wako. Leo tunaendelea kuanzia pale tulipoishia
wiki iliyopita.
Amini
kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo.
Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda
maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda
‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.
Kwa
kawaida, anaweza kuwepo mtu ambaye atakufanya usimuamini mwenzi wako
hata kidogo. Inawezekana akakujengea picha kutokana na maneno ya zamani
au matukio yaliyopita. Je, unaona wivu kwa sababu umeambiwa mpenzi wako
aliwahi kutoka na watu wawili tofauti kabla yako?
Wivu
wa nini? Kwa nini maneno hayo yakuchanganye akili? Je, ulimkuta akiwa
mbumbumbu wa mapenzi na hajawahi kutoka na yeyote? Kumbe utabaini kuwa
historia ya mwenzi wako haina maana inayokubalika kwenye uhusiano
endelevu.
Wanasema
Shetani wa jana, leo anaweza kuwa malaika. Vilevile malaika wa leo
kesho anaweza kuwa Shetani. Inawezekana hao ulioambiwa alitoka nao
walimtenda ndiyo maana hakuwapa nafasi ya kudumu lakini wewe umepata
fursa hiyo kwa sababu unakidhi mahitaji yake. Hata hivyo, hii haina
maana kuwa kila wivu unaotokana na kuambiwa hauna maana. Yapo mengi
yenye maana.
8. MWONESHE MWENZI WAKO
Ukiwa
na mwenzi wako, muoneshe kwa mifano halisi jinsi unavyojisikia au
unavyoweza kumtendea katika nyakati ambazo unamuonea wivu. Kufanya
hivyo, ni rahisi kwake kutambua maumivu yako, vilevile na yeye atajua
mahali ambapo anakosa mengi matamu.
Mtu
anapoona wivu wa ndani, husumbuliwa na maumivu ya moyo. Aghalabu, akili
yake hushindwa kufanya kazi inavyotakiwa. Mantiki ya hoja hiyo ni
kwamba mwenzi wako hawezi kukutendea mambo matamu, ikiwa kichwa chake
hakitakuwa katika hali ya kawaida.
Unaweza
pia kuvuta picha na kujadili muonekano wako pindi unapokuwa na wivu.
Hakikisha mwenzi wako anakuelewa kinagaubaga kile unachomaanisha. Je,
umegundua umepoteza raha kiasi gani? Umefahamu namna ambavyo huwa
unaboa? Mpe uhuru mpenzi wako akwambie ukweli.
Inawezekana
akawa anasita kukwambia bayana kutokana na hofu. Unapaswa kulijua hilo
mapema. Unaweza kumpa nafasi aseme, akakujibu hakuna kitu. Ukishagundua
kuwa anakuhofia, jaribu kumshawishi ili afunguke. Akikubali kueleza la
moyoni, ni tiba kubwa kwako.
Bila
shaka utagundua ni kiasi gani anakerwa na tabia yako ya wivu. Je, ni
nani anapenda kumuudhi mwenzi wake kila siku? Hakuna na kwa hakika hata
wewe mwenyewe hupendi. Hivyo basi, amani yake itatokana na tabia yako ya
kumuonea wivu.
Fikiria
kuwa anashindwa kuwa mtulivu kufanya jambo lolote kwa sababu anahofia
unaweza kulipokea tofauti. Kwa nini unamnyima uhuru kwa sababu ya wivu
wako? Fungua moyo leo, muoneshe kuwa unamuamini. Imani yako itamfanya
aongeze upendo kwako. Siku zote, mapenzi husafiri kwa mtindo wa nipe
nikupe.
Hata
hivyo, njia hii kwa watu wengine hushindwa kufanya kazi. Inapasa mtu
mwenyewe awe amedhamiria kurejesha amani na furaha kwake na kwa mwenzi
wake. Vema uzingatie kwamba wivu ukizidi ni ushamba. Jamii itakudharau,
hata mwenzi wako akikuchoka, anaweza kukugeuza zuzu.
7. JIAMINI
Wivu
mara nyingi huanza kutokana na kukosa kujiamini. Jiulize, unajisikia
salama wewe mwenyewe? Je, unaogopa kwamba mpenzi wako anaweza kukuacha
kwa sababu ya kupungukiwa sifa kadhaa? Mambo mengi kati ya hayo
yanapogota kichwani, huyafanya maisha yako yatawaliwe na wivu.
Inawezekana
mwenzi wako anakupenda kuliko wewe unavyompenda. Si ajabu, akawa
anawaza kufanya maisha bora zaidi akiwa na wewe. Amekukubali kwa namna
ulivyo kiasi kwamba hawazi kukupoteza. Tofauti na mawazo yake, tabia
yako ya kutojiamini, hufikiria kwamba hakupendi.
Ikitokea
akawa anafanya mawasiliano na mtu wa jinsia kama yako, hapo unaanza
kuweweseka, mara ukasirike, upekue simu yake bila sababu, umkaripie,
unune na kususa kuzungumza naye. Hiyo ni kujipa jakamoyo.
No comments:
Post a Comment