Rais wa zamani wa Liberia, Charles
taylor, amehukumiwa kifungo cha miaka 50 jela baada ya kukutwa na hatia
katika kesi iliyokuwa ikiendeshwa dhidi yake ya kuhusika na uhalifu wa
kivita.
Mwezi uliopita, mtawala huyo wa zamani
wa Liberia, alikutwa na hatia ya kuhusika katika kuviwezesha vikundi vya
kigaidi nchini Sierra Leone, na mahakama maalum nchini Sierra Leone,
kupitia kwa jaji wake mmoja imeeleza kuwa hukumu hiyo imeendana na
kiwango cha makosa aliyoyatenda Bw. Taylor.
Taylor mwenyewe kwa upande wake
ameendelea kusisitiza kuwa hakuhusika na tuhuma zilizopelekea kuhukumiwa
kifungo hicho na taarifa za awali zinaeleza kuwa anatarajiwa kukata
rufaa kupinga hukumu hiyo. Mchakato wa kukata rufaa hiyo unaweza
kuchukua hadi miezi sita.
Alikuwepo mahakamani wakati hukumu dhidi
yake ilipokuwa inasomwa, na hakuonekana kushtushwa na lolote lile zaidi
ya kutulia mahali pake alipokuwa amekaa huku akiwa amevalia nadhifu
kabisa suti yake na tai maridadi.
“Mtuhumiwa amekutwa na hatia ya kuhusika
katika kuviwezesha vikundi vya kigaidi katika matukio mabaya kabisa ya
kigaidi kuwahi kutokea katika historia ya dunia hii” alisikika jaji
Richard Lussick akitamka wakati wa usomwaji wa hukumu hiyo ambayo
imekuja baada ya miaka takriban mitano ya usikilizwaji wa shauri
lenyewe.
No comments:
Post a Comment