Pages

Wednesday, June 27, 2012

3000 kukosa udahili vyuo vikuu

 
TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), imesema kuwa wanafunzi 3000 kati ya 40,000
waliomba kujiunga na vyuo mbalimbali nchini wamekosa udahili kutokana na
kasoro mbalimbali.

Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Sifuni Mchome, aliliambia gazeti hili kuwa
wanafunzi 37,000 ndio waliofanya maombi hayo kwa usahihi kupitia mfumo
unaojulikana kama 'Central Admission System', udahili wao una makosa
mbalimbali.

“Jana (juzi) niliangalia na kuona wanafunzi 40,000 ndio wamefanya maombi,
hao 3000 ndio wenye makosa mbalimbali, wengine wameingia tu na kufikiri
ndiyo wameshafanya maombi na makosa mengine kama hayo,” alisema Profesa
Mchome na kuongeza: “Barua pepe ambazo zitakuwa zimewarudia ni vyema
wakazifanyia kazi kabla ya siku ya mwisho ambayo ni Juni 30.”

Alisema kuwa Julai 6 TCU itakutana na vyuo ili kupitia majina ya waombaji
ambapo Julai 15 watakaa na kufanya udahili kamili kwa kuwapangia wenye sifa
kwenye vyuo walivyoomba. “Nawaambia wanafunzi wasubiri huo udahili wa Julai
15,” alisema Profesa Mchome.

Katika hatua nyingine, wakuu wa vyuo na wadau wengine wa vyuo vikuu,
walikutana jana jijini Dar es Salaam kujadili mfumo wa pamoja wa tuzo
(University Qualification Framework). Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
mkutano wa kujadili mfumo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu
Selestine Gesimba, alisema mfumo huo utasaidia kuweka viwango sawa vya
mafunzo yanayotolewa na vyuo vikuu vyote nchini.

Katika hatua nyingine, Profesa Mchome alizungumzia wizi uliotokea katika
ofisi hiyo usiku wa kuamkia juzi akisema kuwa, mali zilizopotea ni kompyuta
10 huku thamani yake ikiwa haijajulikana.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment