Pages

Sunday, July 8, 2012

Atakayeleta medali Olimpiki kuzawadiwa mil. 13.2/-



WAKATI timu ya Tanzania itakayoshiriki michezo ya Olimpiki London, Uingereza ikitarajiwa kuondoka leo, mchezaji atakaye twaa medali atapewa zawadi ya sh mil. 13.5.

Hayo yalibainishwa juzi na wadau na Kamati ya Olimpiki Tanzania, (TOC), jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuiaga timu hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola, katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, sasa Hyajatt, ambako mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.

Wa kwanza kutoa ahadi hiyo ni Mkuu wa Majeshi wa zamani na Waziri mwenye dhamana ya michezo, Jenerali mstaafu, Mrisho Sarakikya, aliyeahidi dola 2,000 za Marekani kwa atakayerejea na medali.

Aidha, Kamati ya TOC chini ya Rais wake, Ghulam Rashid na Katibu Mkuu, Meja mstaafu, Filbert Bayi, nayo iliongeza dau la sh milioni 10.

Nyota watakaoiwakilisha Tanzania katika fainali hizo ni nahodha Samson Ramadhani, Faustine Mussa, Msenduki Mohamed, Zakia Mrisho (riadha), Suleiman Kidunda (ngumi za ridhaa), na Magdalena Moshi (kuogelea).

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri Makalla, aliwataka wachezaji kujituma na kutambua umuhimu wao, kwani wamebeba dhamana ya Watanzania takriban milioni 40 kupeperusha bendera ya Tanzania.

Aliwaasa kwenda kulipigania taifa na kwamba, matatizo kila siku rafiki yake ni yatima na mafanikio huwa anapendwa na wengi, hivyo kuwataka kufanya vema katika mashindano hayo ili wapate marafiki wengi na kuungwa mkono zaidi.

Aidha, Waziri Makalla alimpongeza Rais wa zamani wa Chama cha Riadha Tanzania, (RT), Francis John, kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa kwa timu hiyo na kumtaka aendelee na moyo huo.

Pongezi hizo pia zimekwenda kwa TOC kwani licha ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu, kwa kushirikiana na vyama vya michezo vilivyotoa wachezaji wa kwenda Uingereza.

Aidha, Waziri Fenella Mukangara, anatarajia kuungana na timu ya Tanzania waliofuzu kwa fainali hizo zitakazoanza baadaye mwezi huu.

No comments:

Post a Comment