Pages

Monday, July 30, 2012

JOGOO MWENYE SHANGA, HIRIZI AZUA KIZAZAA


 
Na Salum Maige, Sengerema

WAKAZI wa Mtaa wa Nyanchenche Road mjini Sengerema juzi walifurika kushuhudia tukio la kuonekana jogoo asiye na manyoya akitembea huku akiwa amefungwa shanga na hirizi mbili shingoni na mabawa yake yakiwa yamechanjwa chale na kupakwa dawa nyeusi.
 
Tukio hilo lililovuta umati wa watu lilitokea juzi  saa 7:00 mchana kwenye moja ya familia ya mtaa huo[jina limehifadhiwa]ambaye alidai kwamba kuku huyo alijitokeza nyumbani kwake bila kufahamu alikotokea.
 
Kuku huyo wa ajabu alikutwa na wananchi katika mji huo ulioko kando kando ya barabara,jambo lililowashtua wakazi wa Sengerema waliofika kulishuhudia huku wakilihusisha na imani za kishirikina.
 
Katika tukio hilo hakuna mwananchi aliyejitokeza kumshika kuku huyo, huku wenyeji wa mji husika wakiendelea na shughuli zao licha ya kuonyesha mshituko.
 
Akizungumza na waandishi wa habari,Mwenyekiti  wa kitongoji hicho Leah James alieleza kushangazwa na tukio hilo aliloliita la ajabu, na kwamba halijawahi kutokea  katika kitongoji hicho kwani limeibua hisia tofauti miongoni mwa wanajamii.
 
“Nimepata taarifa za tukio hili ilikuwa mchana muda wa saa saba na tumefika mpaka eneo la tukio, kwa kweli inashangaza na kusikitisha, huyo kuku wa ajabu hana nyoya hata moja wala alama ya kidonda na amechanjwa chale kwenye mbawa zake,kavishwa hirizi mbili shingoni na amefungwa shanga kwenye mbawa zake” alisema mwenyekiti.
 
Baada ya tukio hilo uongozi wa eneo hilo na sungusungu uliamua kuitisha mkutano siku iliyofuata leo(jana) ambapo walifuatilia na kumbaini mmiliki wa kuku huyo kuwa ni  Leticia Makoye ambaye alidai kuku huyo ni wake na  humtumia katika shughuli za uganga wa kienyeji .
 
Kikao hicho kiliamua kumrudishia kuku huyo ingawa alikuwa tayari amekufa kutokana na kupigwa baridi usiku kucha, maamuzi yaliyopingwa na wananchi na hivyo kulazimika kumshambulia kwa mawe hadi nyumbani kwake huku viongozi wa mtaa huo wakimpatia ulinzi hadi alipoingia ndani ya nyumba.
 
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Gazeti hili eneo la tukio wamekuwa na hisia tofauti huku baadhi yao wakilihusisha na imani za kishirikina kutokana na vitu alivyokutwa navyo kuku huyo ikiwa ni pamoja na shanga,hirizi,na chale alizochanjwa kwenye mbawa zake.
 
Grece Michael (32), Fadhili Alfani (45), na Daniel Marco walisema  matukio ya ajabu kama hilo ni dalili za mwisho wa dunia kutokana na vitendo vya kishirikina kuongezeka na kwamba njia pekee ya kuepukana navyo ni kudumu katika sala na imani.

Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment