MABADIKO
ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012, iliyopitishwa
Aprili mwaka huu, imeendelea kuzua mtafaruku sehemu mbalimbali nchini,
huku wabunge wakishinikiza kuwa, sheria hiyo inapaswa kurejeshwa bungeni
ili ijadiliwe upya.
Jana,
wabunge waliunga na wafanyakazi kupinga kipengele cha sheria hiyo
kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao yake baada ya kufikisha umri wa
kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, au miaka 60 kwa mujibu wa sheria.
Hoja
ya kutaka suala hilo lijadiliwe upya ilitolewa na Mbunge wa Kisarawe
(CCM), Selemani Jafo ambaye aliungwa mkono na Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni
Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama.
Hoja
ya Jafo ilitokana na kuwapo kwa taarifa kuwa, zaidi ya wafanyakazi
600 katika migodi minane nchini wameacha kazi huku wengine zaidi ya
4,000 wakiwa tayari wamewasilisha barua za kuacha kazi kutokana na
sheria hiyo.
Hata
hivyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alitofautiana na wenzake
pale aliposema kuwa sheria inayolalamikiwa ilishapitishwa na Bunge,
hivyo angependa kujua uhalali wa kujadiliwa tena bungeni.
Jijini
Dar es Salaam, mjadala mzito uliendelea huku baadhi ya wanasheria
waliozungumza na gazeti hili wakisema: “Marekebisho hayo ni kandimizi na
yanalenga kuwanyima haki wanachama ambao wanaweza kupata matatizo
mbalimbali wakiwa kazini”.
Kwa
upande wake Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA), jana ilitoa taarifa iliyoweka bayana kuwa, fao la kujitoa
kazini limefutwa na kwamba jambo lolote linalohusu mafao ya aina hiyo
linapaswa kusubiri kutolewa kwa miongozo husika.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment