Pages

Sunday, July 8, 2012

VIONGOZI WA DINI WATAKA KUKUTANA NA RAIS JAKAYA KIKWETE PAMOJA NA MADAKTARI ILI KUTAFUTA UFUMBUZI WA MGOMO


NA MWANDISHI WETU    

VIONGOZI wa dini nchini, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kukutana nao wakiwemo madaktari, ili kulitafutia ufumbuzi suala la mgomo wa madaktari linaloendelea na kuwatesa wananchi wasio na hatia.

Kauli hiyo imetolewa  jijini Dar es Salaam jana, na Sheikh Said Mwaipopo wakati wa kutoa tamko la pamoja juu ya maamuzi yao.

Alisema wamechukua hatua hiyo, baada ya kubaini kuwa serikali inasuasua kulizungumzia jambo hilo kwa makini na kulipatia ufumbuzi ili kuokoa maisha ya watu wa kipato cha chini wanaotegemea hospitali za serikali.

“Kuna mambo mbalimbali yanaweza kutokea, inawezekana taarifa sahihi hazimfikii waziri, hivyo tunaomba kukutana naye kwa mazungumzo ya amani ili kurudisha hali ya amani nchini” aliongeza Mwaipopo.

Sheikh Mwaipopo alifafanua kuwa tamko lao limejigawa katika  sehemu kuu tano, ambapo wanaamini kukutana huko kunaweza kuwa ishara ya kumaliza mgogoro unaowakabili na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.

Aidha, alichanganua kuwa tamko lao la kwanza litaiomba Serikali kufuta kesi iliyoko mahakamani, iwarejeshe madaktari wote walioachishwa kazi, Rais kukubali kukutana na viongozi wadini, sanjari na wanaharakati wa haki za binadamu.

Naye Mchungaji wa EAGT Mabibo, Lawrence Mzavaz alisema hawahusiki na tuhuma zinazovumishwa kuhusu tukio lililotokea la Dk Ulimboka kwasababu hakuna aliyeshuhudia uovu huo unavyofanyika.

Alisema tamko lao halitakubaliana na kauli ya aina yeyote itakayo wataka wananchi kuandamana kwani wanaamini hiyo siyo njia sahihi ya kumaliza tatizo lililopo.

Aidha, Mch. Mzavaz alisema iwapo Rais atashauriwa vibaya na kukataa kukutana na umoja wa viongozi hao, hawatakuwa na la kufanya kwa sababu maamuzi hayo yatakuwa yamefanywa na kiongozi wan chi.

No comments:

Post a Comment