Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, August 25, 2012

KATIBU WA CHADEMA MKOA WA MOROGORO AJIUZULU



Katibu wa Chama cha Damokrasia na Maendeleo Mkoani Morogoro, Abel Luanda ametoa tamko rasmi la kujiuzu nafasi hiyo na kuahidi kutoa taarifa ya chama atakachohamia mapema wiki ijayo.
Luanda alitoa tamko hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kutaja sababu tano zilizomsababisha kuchukua maamuzi hayo aliyoyaita kuwa ni magumu katika siasa.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni kupisha upepo mbaya wa kisiasa ndani ya Chadema kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa, kukosa ushirikiano na mwenyekiti wa Chadema mkoa Susan Kiwanga ambaye ni mbunge wa viti maalumu wa chama hicho mkoani hapa pamoja na dharau iliyojengwa na viongozi wakuu wa chama hicho kitaifa dhidi ya viongozi wa mkoa.
Sababu nyingine alieleza kuwa ni kupisha agenda ya siri iliyofichika ndani ya M4C inayolenga kuwaondoa viongozi fulani ndani ya mkoa na wilaya wanaoonekana kuwa na misimamo ya kupinga kambi fulani inayojiandaa na uchaguzi mkuu wa chama hapo mwakani.
Vilevile alisema kuwa sababu iliyomfanya ajiuzulu ni pamoja na viongozi wa ngazi ya chini kuanzia kata, jimbo, wilaya hadi mkoa kutumiwa kama muhuri huku wakitakiwa watimize wajibu mkubwa wakati mtetezi wa haki zao hayupo.
“Mimi naondoka lakini nawaachia ujumbe mmoja kuwa Chadema siyo yenu ninyi viongozi wachache ambao mpo hapa kwa dhamana tu nanyi mtapita kama waasisi wa chama hichi waliopita, lakini nawaachia chama kikiwa salama na imara” alisema Luanda.
Aidha alisema kuwa yeye si mgeni kwenye siasa kwani aliwahi kuwa mwanachama wa NCCR- Mageuzi na baadaye alihamia Chadema na kupata nafasi ya udiwani mwaka 2005-2010 wa kata ya Kibungo juu ambapo alisema kuwa katika nafasi hiyo aliweza kukiimarisha Chadema kuanzia ngazi ya tawi hadi mkoa.
Alisema kuwa kutokana na mema aliyoyafanya kwa Chadema anaamini kuwa wapo viongozi wengine wa chadema wa ngazi mbalimbali watakaounga mkono maamuzi yake na kuachia ngazi hivyo aliwataka kutoogopa kukihama chadema kwani wanaweza kufanya siasa kwenye chama chochote.
Alipotakiwa kueleza kama anania ya kuhamia CCM Luanda alisema kuwa kwa sasa anaangalia upepo wa kisiasa na muda si mrefu atatangaza ramsi chama atakachohamia huku akisisitiza kuwa atahamia chama ambacho kitakuwa na misimamo na chenye kufuata katiba na miongozo na sio kupigana majungu na fitina.

No comments:

Post a Comment