Pages

Sunday, August 12, 2012

Mbuyi Twite amng’oa Rage TFF



SAKATA la beki Mbuyi Twite wa APR ya Rwanda kudaiwa kunyakuliwa na watani zao, Yanga, limechukua sura mpya baada ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, kuamua kubwaga manyanga nafasi yake ya ujumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa madai ya kuikandamiza klabu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Rage alisema, kamati hiyo ni miongoni mwa taasisi za TFF, zinazoikandamiza Simba.
Rage alisema, Twite alisaini mkataba wa miaka miwili na Simba na alilipwa dola 30,000 za Kimarekani, lakini wakati wakisubiri kupewa barua ya kumruhusu kutokea APR, wamepata taarifa za kuchanganya kutoka Rwanda kuwa, mchezaji huyo amesaini mkataba na Yanga.
Alifafanua kuwa, wamepata taarifa kutoka APR kuwa, hawawezi kumruhusu mchezaji huyo kuchezea Simba, kwa sababu wamezuiwa na mtoto wa kigogo, ambaye hakumtaja jina - ila anafahamika.

"Nasema kweli na hapa nimefunga (mwezi mtukufu wa Ramadhani), tumepata taarifa kutoka APR kuwa, kuna mtoto wa kigogo wa serikali kutoka Tanzania, amemzuia mchezaji huyo kutua Msimbazi...
"Sitaki kumkisia mtu yeyote vibaya na sitasema jina la mtoto huyo wa kigogo wa juu wa serikali...mchezaji analazimishwa kutoichezea Simba na kupelekwa timu ya kigogo huyo pasipo kufuata taratibu za soka.
"Huu ni uonevu mkubwa tuliofanyiwa kwa jumuia ya wapenda michezo kwa ujumla na hali hii inaonesha wazi kuwa, mchezo wa soka hapa nchini unaelekea kubaya," alisema huku akitokwa na machozi.
Alisema, mtoto huyo wa kigogo amekuwa akitajwa mara kwa mara kwenye tuhuma za kurubuni wachezaji wa Simba kujiunga na Yanga.
Rage alisema, vitendo vya aina hiyo vya kutumia mamlaka ya mtu, yawe ya kiserikali au kifedha, ni kinyume cha taratibu, pia ni hatari kwa maendeleo ya soka nchini.
"Sitapenda kuwa Mwenyekiti wa Simba wakati mashabiki wa klabu yangu na watani wetu wa jadi watakapogeuka kuwa maadui...huku tunakokwenda sasa ni kwenye kujenga uadui, chuki na kinyongo baina ya mashabiki wetu," alisema.
Alisema, Simba haitakubali kuona Twite akisajili kuichezea Yanga au timu nyingine yoyote Tanzania kwa namna yoyote ile, kwani amesajiliwa na Simba na mkataba wake upo.
Hata hivyo, alisema, kutokana na mchezaji huyo kutokuwa mwaminifu, Simba inamtaka arejeshe fedha alizochukua, ikiwemo gharama ya usafiri na mali ambazo walitumia kwenda Rwanda.
Aliongeza kuwa, Simba inaitaka serikali kuwa makini katika suala hilo na kwamba, kitendo kilichofanywa na Yanga kupitia mtoto huyo wa kigogo, kitahatarisha amani na utulivu wa nchi.
"Naomba niseme wazi, kwenye hili Simba haitaacha kupambana hata kwa dakika moja, na kama busara itashindwa kuchukua mkondo wake, suala hili nitalipeleka kwa wanachama wetu ili waamue watakavyo," alisema.
Wakati tunakwenda mitamboni, kulikuwa na habari kuwa wawakilishi wa mchezaji huyo kutoka DR Congo, wametua nchini jana kurejesha fedha za Simba kiasi cha dola 30,000 za Marekani ambazo zimekabidhiwa kwa TFF.
SOURCE TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment