KIKOSI
cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kikiwa na wachezaji
17 kimewasili leo asubuhi jijini Gaborone tayari kwa mechi ya kirafiki
ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya
wenyeji Botswana 'Zebras' itakayochezwa kesho.
Stars
ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama saa
5.45 asubuhi kwa saa za hapa ambapo nyumbani ni 6.45 na kupokewa na
viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania
wanaoishi hapa Botswana.
Baadhi
ya wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank Domayo, Ramadhan
Singano na Simon Msuva ambao walijiunga na Stars saa chache baada ya
kurejea kutoka Nigeria ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri
chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya
mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).
Wachezaji
wengine kwenye kikosi kilichoko Botswana ni Aggrey Morris, Amir Maftah,
Athuman Idd, Erasto Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja, Kelvin Yondani,
Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo, Salum
Abubakar, Said Bahanuzi na Shabani Nditi.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia kwenye hoteli ya
Oasis ambayo pia ndipo Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi hiyo.
Mechi itaanza kesho saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na itafanyika
kwenye Uwanja wa Molepolole Sports Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana
hivi sasa uko kwenye matengenezo.
Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema mechi hiyo ni muhimu kwa vile
timu yake bado inakabiliwa na mechi za Kombe la Dunia Kanda ya Afrika,
na michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)
inayotarajia kuanza baadaye mwaka huu.
SOURCE BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment