Pages

Saturday, September 1, 2012

WATATU MBARONI MKOANI IRINGA KWA WIZI WA NG’OMBE



Jeshi la polisi mkoani Iringa linawashikilia watu watatu wakazi wa mkoani hapa kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio la wizi wa ngombe ambalo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 27 mwaka huu.
Kamanda wa polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Onesmo Ndondole, mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa kijiji cha Kitelewasi, Titus Amon, umri miaka 25, mkazi wa Itimbo, wilayani Kilolo na Isaya Muyinga mwenye umri wa miaka 18, mkazi wa Kigonzile, manispaa ya Iringa.
Kamanda Kamhanda amesema baada ya kufanyika kwa upelelezi jeshi la polisi limefanikiwa kuwapata ng’ombe 4, kati ya saba ambao wameibiwa.   
Kamanda Kamhanda ameongeza kuwa mifugo hiyo ni mali ya Bw. Julius Mhandisi, mkazi wa Ilula wilaya ya Iringa vijijini, ambao waliibiwa majira ya usiku wakiwa kwenye zizi.
Wakati huo huo, watu wawili wamefariki kwenye matukio mawili tofauti likiwemo la kupigwa na watu wasiofahamika na miili yao kutelekezwa njiani ikiwa na majeraha sehemu za kichwani.
Kamanda wa polisi amemtaja Dicto Mballa, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa kijiji cha Ugenza, amefariki baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.
Katika tukio la pili Kamanda Kamhanda amesema Jutindus Kipesile, mwenye umri wa miaka 38, mfanyabiashara wa kinyanambo B, amefariki baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mwili wake kutelekezwa njiani.
Hata hivyo hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na matukio hayo, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watuhumiwa wa matukio hayo na watuhumiwa wa wizi wanatarajia kufikishwa mahakani kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment