KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad
Slaa, amemvaa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya
Kikwete, akisema amekitengenezea kaburi la kukizika rasmi chama chake
kwa kuruhusu watuhumiwa wakubwa wa ufisadi kugombea nyadhifa mablimbali.
Dk. Slaa
alisema uteuzi wa wagombea ndani ya CCM uliomalizika juzi umeonyesha
wazi kwamba sasa chama hicho kinatumbukia kwenye dimbwi kubwa na pana
lisiloweza kukitoa tena.
Akizungumza
na Tanzania Daima jijini Mwanza, alikojichimbia kuhakikisha mchakato wa
uchaguzi wa mameya wa jiji hilo unakwenda vizuri leo, Dk. Slaa alisema
dhamira ya kweli dhidi ya CCM katika kuwaweka vijana kwenye uongozi ili
kukinusuru chama hicho imezimika baada ya Kikwete kuruhusu watuhumiwa wa
ufisadi na wakongwe kugombea uongozi.
“Katika
hili la uteuzi wa CCM, nangojea taratibu zao zikamilike. Tulitegemea CCM
muda huu ni wa kujisafisha, lakini imeshindwa kufanya hivyo. Mimi
simung’unyi maneno kuhusu watuhumiwa wa ufisadi.
Mfano
(anataja) ni fisadi wa fedha za rada. Mimi hapa nilishapeleka ushahidi
hadi wa akaunti namba ya benki yake kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka
Nchini), alisema.
Alisema
inashangaza kuona katika utetezi wa CCM, mtuhumiwa huyo amepatiwa nafasi
licha ya kushindwa kueleza wazi fedha nyingi kwenye akaunti hiyo ya
Uswisi alizipataje.
“Mtuhumiwa
mkubwa kama huyu wa ufisadi eti leo CCM inampitisha awe mgombea. Kweli?
Sioni dhamira ya CCM kupambana na vitendo vya kifisadi. Na hata dhamira
ya vijana haipo bali imejitumbukiza kwenye dimbwi ambalo kamwe
hakitatoka humo,” alisisitiza.
Kuhusu
Lowassa na tuhuma zake za ufisadi wa kampuni ya kufua umeme wa dharura
wa Richmond zilizosababisha kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, Dk. Slaa
alisema kiongozi huyo alilazimika kujiuzulu kama sehemu ya kuwajibika,
lakini ameshindwa hadi leo kumtaja mhusika hasa wa kampuni hiyo.
Alisema
kama kweli Lowassa alisingiziwa katika tuhuma hizo, alipaswa kuwaeleza
Watanzania nani anayehusika na ufisadi huo wa Richmond ambayo ilishindwa
kuzalisha umeme licha ya kutumia mamilioni ya fedha za umma.
Kuhusu
wanachama wa CCM ambao majina yao yamekatwa na NEC, Dk. Slaa alisema
milango iko wazi CHADEMA kwa wale wasio mafisadi kujiunga ili
kukielekeza chama hicho kushika dola mwaka 2015.
Alisema
CHADEMA ni chama makini huenda kuliko vyama vingine, hivyo hakiwezi
kupokea wanachama kutoka CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi, vinginevyo
kitafunga milango na mapazia yake.
“Unajua,
kuna watu wanaojulikana kwa ufisadi. Pia wapo wasafi wanaoomba kujiunga
na CHADEMA, hivyo watu safi hawana tatizo kujiunga na CHADEMA kwa ajili
ya kuunganisha nguvu kwenda kuongoza dola mwaka 2015,” alisema Dk. Slaa.
Mnyukano wa umeya
uchaguzi
wa mameya wa wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza,
unatarajiwa kufanyika leo huku mnyukano mkali ukiwa katika halmashauri
ya Nyamagana kutokana na CCM na CHADEMA kuwa na idadi sawa ya viti vya
madiwani na hivyo kutegemea kura za CUF ziamue mshindi.
Katika
Halmashauri ya Ilemela, CHADEMA ina uhakika wa asilimia mia moja
kutokana na kuwa na madiwani wengi kuzidi wenzao wa CCM huku mikakati
yao ikilenga kuwashirikisha CUF ili waitwae pia Nyamagana.
Uchaguzi
huo unafanyika baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kugawanywa na
hivyo kuzaa halmashauri hizo mbili. Lakini pia Halmashauri ya Jiji la
Mwanza kwa sasa muda kadhaa haikuwa na Meya baada ya Baraza la Madiwani
kumvua wadhifa huo, Jackson Manyerere (CHADEMA).
Baada ya
meya kuenguliwa, kulizuka mtafaruku ndani ya CHADEMA jijini hapa ambao
ulisababisha madiwani wawili kutimuliwa uanachama kwa kile kilichodaiwa
ni usaliti wa kuanzisha hoja ya kumtosa kiongozi huyo.
Hivyo
kutokana na CHADEMA kutokuwa na madiwani hao, inaingia kwenye uchaguzi
wa leo ikiwa na madiwani sita na mbunge Ezekiel Wenje katika wilaya ya
Nyamagana wakati wenzao CCM wana madiwani saba na CUF wawili.
Kwa
mnyukano huo ni dhahiri kuwa CHADEMA na CCM watakuwa wamefungana kwa
kura na hivyo kuhitaji huruma ya madiwani wa CUF ili upande mmoja uibuke
kidedea.
Taarifa
za uhakika kutoka jijini hapa ni kwamba CHADEMA wamefanya mazungumzo ya
kushirikiana na CUF kwa kuwaachia nafasi ya Naibu Meya ambayo itagombewa
na diwani wao wa kata ya Mirongo, Daud Mukama.
Kwa
halmashauri ya Ilemela CHADEMA wana uhakika wa kuibuka kidedea kutokana
na kuwa na madiwani wanane na mbunge Highness Kiwia huku wenzao wa CCM
wakiwa na madiwani sita na CUF ina mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa
Kimwanga.
Kamati za
utendaji za CHADEMA katika wilaya hizo zimefanya vikao tofauti kwa
kushirikiana na kamati za madiwani na kukamilisha mchakato wa kupata
wagombea wao.
Kwa
mujibu wa ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, kamati ya utendaji ya
wilaya pamoja na madiwani wa Nyamagana walimteua aliyekuwa Naibu Meya
kabla, Diwani wa Kata ya Maina, Charles Chibara, kuwa mgombea wa umeya
wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Kwa
upande wa Ilemela, kikao cha kamati ya utendaji pamoja na madiwani
walimteua Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera, kuwa mgombea wa
umeya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Kikao
hicho cha Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny Kahungu, kuwa
mgombea wa nafasi ya Naibu Meya halmashauri hiyo wakati kamati ya
utendaji ya Nyamagana imekubali kumwachia kugombea nafasi ya Naibu Meya
wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diwani wa Mirongo, Daudi Mkama (CUF).
Wao CCM
wamemteua Diwani ya Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kugombea nafasi
ya umeya katika halmashauri ya jiji la Mwanza huku diwani wa kata ya
Igogo, John Minja, akigombea unaibu meya na Ilemela wagombea ni Renatus
Kalunga na naibu wake Sarah Ng’hwanu.
SOURCE TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment