SIKU
chache baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kulitupilia mbali
ombi la Shirika la Ugavi wa Umme nchini (TANESCO) la kutaka izuie
utekelezwaji wa ulipwaji wa fidia ya Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd,
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema mafisadi
waliohusika ndio wabebeshwe hasara hiyo badala ya wananchi.
Juzi,
mahakama hiyo, ilitupa ombi la TANESCO lililokuwa likiomba itoe amri ya
kuzuia utekelezwaji wa ukazaji wa hukumu ya mahakama hiyo iliyoruhusu
tuzo ya dola 65,812,630.03 za Marekani iliyotolewa na Mahakama ya
Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) mwaka 2010 kwa
Kampuni ya Dowans Hodlings SA (Costa Rica), sasa Dowans Tanzania Ltd
isajiliwe hapa nchini.
Mnyika
ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), alitoa kauli hiyo jana
kupitia taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari akisema kuwa
serikali isitumie kizingizio cha uamuzi wa mahakama kuharakisha mpango
wa kulipa Dowans kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania.
Vile
vile, Mnyika alisema kuwa ikiwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete
imezidiwa na Dowans kwa sababu ya kujiingiza katika mikataba mibovu,
inapaswa kuwabebesha deni hilo wazembe, mafisadi na waliokuwa
wakihujumiana na kusababisha hasara hiyo.
“Serikali
kupitia Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, anapaswa
kueleza ni hatua gani ilichukua kutoka TANESCO ilipowasilisha Mahakama
ya Rufani taarifa ya kusudio la kupinga hukumu iliyotolewa na Jaji
Emilian Mushi, Septemba 28 mwaka jana ikiruhusu tuzo hiyo isajiliwe,”
alisema.
Aliongeza
kuwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye anapswa kueleza ni kiasi gani
cha fedha kilichotumika kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka
sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni
binafsi yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi
ambazo serikali inashindwa.
“Ni
muhimu umma ukafahamu kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee, jumla ya
sh bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi hizo
kwa kuilipa Kampuni ya Rex Attorneys na makampuni mengine ambayo kwa
nyakati mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha serikali na TANESCO,” alisema
Mnyika.
Alishauri
kuwa hukumu ya juzi inapaswa kuibua tena mjadala uliodumu kwa miaka
minne, kuanzia mwaka 2008 tangu yalipopitishwa maazimio 23 ya Bunge juu
ya mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company
LLC ikiwamo kuhusu mkataba na Dowans.
Alisema
katika mazingira hayo, Waziri Muhongo anapaswa kueleza kwa umma ni
mabilioni mangapi yamelipwa na TANESCO mpaka hivi sasa kwa kampuni hiyo
na nyingine.
“Kama
hoja binafsi niliyoiwasilisha ofisi ya Bunge mwaka jana kutaka
utekelezaji wa maazimio yote yaliyobaki kuhusu mkataba kati ya TANESCO
na Richmond ingejadiliwa bungeni, hatua zaidi zingechukuliwa kwa
mafisadi na wahujumu uchumi waliohusika,” alisema Mnyika ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.
No comments:
Post a Comment