WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Rais asiyekuwa na wizara maalumu na Mbunge wa Jimbo
la Rungwe Mashariki, Prof. Mark Mwandosya, amesema kuwa kifo cha
mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, aliyeuawa na polisi kiwe cha
mwisho.
Kauli
ya Waziri Mwandosya inafuatia mahojiano ya moja kwa moja yaliyofanywa
na Tanzania Daima Jumapili katika Kijiji cha Busoka, Kata ya Itete
mkoani Mbeya ambapo alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliojitokeza
kumzika mwandishi huyo.
Prof.
Mwandosya akiwa anatokea nyumbani kwake katika Kijiji cha Lufilyo
ambapo yupo katika mapumziko ya kiafya, aliweza kujikongoja hadi msibani
hapo huku afya yake ikiendelea kuimarika zaidi na hakuacha kusema yale
ambayo yamemgusa juu ya kifo hicho.
“Hii
inaniuma sana, watoto wadogo tuliowazaa tunashuhudia wakifa hivi hivi,
mazingira ya kifo hiki yamenisikitisha sana, naomba kifo cha Mwangosi
kiwe cha mwisho, sipendi kusikia tena mambo kama haya yakitokea tena,
iwe mwisho, iwe mwisho kabisa,” alisema Prof. Mwandosya.
Licha
ya waziri huyo kuonyesha huzuni na majonzi makubwa juu ya kifo hicho,
alidai kuwa msiba huo ni changamoto kwa serikali, wananchi na viongozi
wa vyama vya siasa kuwa ipo haja ya kujitathimini zaidi juu ya hali ya
nchi ilivyo na ulinzi na usalama wa raia unavyozidi kulegalega.
“Tangu
tupate uhuru miaka 50 iliyopita enzi za Mwalimu Nyerere haya mambo
hayakuwepo, nchi ilikuwa na heshima kubwa na Mtanzania alisifika na
kuheshimika popote duniani anakokwenda. Leo hii tunakwenda wapi?
Tukienda nje tutaambiwa hawa wanatoka kwenye nchi ya vurugu,” alisema
Mwandosya.
No comments:
Post a Comment