Pages

Thursday, October 4, 2012

Bei Ya Petroli Yashuka




 MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei kikomo mpya ambazo zitaanza kutumika leo nchini kote ikiwa imeshuka kwa Sh 306, kwa lita ya petroli, Sh 192 kwa lita moja ya dizeli huku mafuta ya taa bei ikibaki bila kubadilika.

Taarifa iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, ilisema bei za mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam itakuwa Sh 1,994 kwa lita moja ikiwa imeshuka kutoka Sh2,300 ya bei ya Septemba. Alisema mafuta ya dizeli bei yake imeshuka hadi kufikia Sh1,950 kutoka Sh2,142, wakati mafuta ya taa yanabakia Sh1,993 kutokana na kutoingia meli yoyote ya mafuta hayo.

Taarifa hiyo ilisema bei hizo, zitaendelea kuongezeka kutokana na gharama za usafirishaji kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, ingawa kwa ujumla katika kila eneo punguzo litakuwa ni Sh 306 na Sh 192 kwa petroli na dizeli kwa kila lita moja. “Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,”alisema na kuongeza; “Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta kulingana na bei anayoiona mteja inamfaa.”

 Kaguo alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziwe chini ya bei kikomo na kama mfanyabiashara atakiuka atapewa adhabu ya kulipa Sh3 milioni. Pia alivitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana ili mteja afanye uchaguzi wa kununua mafuta akiwa anajua bei halisi ya mafuta katika kituo husika. “Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita kwani stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha ununuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa,” aliongeza Kaguo.

 Hivi karibuni Baraza la Ushindani wa Haki (FCC), lilitupilia mbali rufani ya kampuni 13 zinazojishughulisha na uuzaji wa mafuta, zilizokuwa zinapinga kanuni mpya ya kukokotoa bei za mafuta iliyobuniwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura). Katika hukumu hiyo iliyotolewa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa baraza hilo, Razia Sheikh, alisema uamuzi wa kuitupa rufani hiyo ulitokana na warufani, kushindwa kuthibitisha madai yao kikamilifu.

Alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, baraza liliridhika kuwa Ewura ilikuwa imefuata taratibu zote zilizowekwa kisheria, kabla ya kutangaza kanuni mpya za kukokotoa bei za mafuta nchini. Katika usikilizaji wa shauri hilo, Mwenyekiti Sheikh alisaidiwa na wajumbe wawili ambao ni Malima Bundala na Ali Juma.

 Kampuni zilizokata rufaa ya kupinga uamuzi wa Ewura ni pamoja na BP Tanzania Limited, Engen Petroleum Tanzania Limited, Camel Oil Tanzania Limited, Oilcom Tanzania Limited, Total Tanzania Limited, Gapco Tanzania Limited na Hass Petroleum Tanzania Limited. Nyingine ni Orxy Oil Company Limited, MSG International Tanzania Limites, GBP Tanzania Limited, Lake Oil Limited, Moil Tanzania Limited and Acer Petroleum Tanzania Limited. Pamoja na kutupilia mbali rufani hiyo, Sheikh pia aliziamuru kampuni hizo kulipa gharama za kesi.

Kwa mujibu nyaraka za baraza hilo, gharama za mawakili wa Ewura peke yake ni zaidi ya Sh100 milioni. Pamoja na mambo mengine, kampuni hizo zililiomba baraza hilo kuifuta kanuni hiyo mpya kwa vigezo kuwa, Ewura haikufikiria mambo kadhaa kabla ya kuitangaza.

                    Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment