Aliyekuwa
rais wa Algeria kwa miaka mingi, Chadli Bendjedid, ambaye anasifika kwa
kuanzisha mfumo wa utawala wa kidemokrasia katika taasisi za kiserikali
nchini humo, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 83.
Ripoti
zinasema Bendjadid, aliaga dunia kutokana na maradhi ya saratani baada
ya kulazwa katika hospitali ya kijeshi ya Ain Naajda mjini Algiers tangu
wiki iliyopita.
Januari
mwaka huu, Bendjadid, alipelekwa nchini Ufaransa kwa matibabu ya
saratani na tangu wakati huo amezuru hospitali mara kadhaa.
Bendjadid
ameandika vitabu kadhaa vya kumbukumbu ambayo vinatarajiwa kuchapishwa
tarehe Mosi mwezi ujao, siku ambayo raia wa nchi hiyo wanaadhimisha
kumbukumbu ya kuanza kwa vita vya uhuru wa taifa hilo.
Alihudumu
kama rais wa Algeria, tangu mwaka 1979 hadi mwaka wa 1992 na
kuandikisha historia ya kuwa rais wa nchi hiyo aliyehudumu kwa kipindi
kirefu zaidi.
Bendjadid
aliondolewa madarakani wakati jeshi la nchi hiyo lilipoingilia kati
kuzuia ushindi wa wapiganaji wa Kiislamu, katika uchaguzi wa kwanza wa
vyama vingi nchini humo.
Kufuatia
uamuzi huo wa jeshi wa kuingilia kati masuala ya kisiasa, vita vikali
vilizuka nchini humo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki mbili.
Bendjedid
alikuwa miongoni wa wapiganaji wa uhuru wa taifa hilo kutoka kwa
utawala wa kikoloni kati ya mwaka wa 1954 na mwaka wa 1962 na aliteuliwa
kuwa kamanda wa jimbo la Oran Magharibi mwa nchi hiyo kwa miaka 14.
Alijiunga
na vugu vugu la mapinduzi, lililoundwa Juni mwaka wa 1965, kumuondoa
madarakani rais wa kwanza wa nchin hiyo Ahmed Ben Bella.
Huku
akiungwa na jeshi la nchi hiyo, Bendjedid, alichaguliwa kuwa rais wa
mwaka wa 1979 na mwaka wa 1989 alichaguliwa tena kwa muhula mwingine,
miezi miwili tu baada ya ghasia na machafuko za kulalamikia kuongezeka
kwa bei ya bidhaa muhimu na pia kuitisha kuanzishwa kwa utawala wa
kidemokrasia.
Bendjedid
anasifika kwa kuanzisha utawala wa kidemokrasia nchini humo pale
alipoidhinisha mabadiliko ya kikatiba Februari mwaka wa 1989.
Lakini
baada ya kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, rais huyo
wa zamani alihukumiwa kifungo cha nyumbani katika eneo lake la Oran,
mwaka wa 1992.
Hukumu hiyo ilifutiliwa mbali wakati rais Abdelaziz Bouteflika alipochaguliwa rais mwaka wa 1999.
Bendjedid alizaliwa Aprilo 14, 1929 katika eneo la Bouteldja, Mashariki mwa Algeria karibu na mpaka wa Tunisian.
No comments:
Post a Comment