Rais Mwai Kibaki wa Kenya amepinga jaribio la wabunge nchini humo kutaka kujizawadia posho ya ziada ya zaidi ya dola za Marekani 105,000 kila mmoja.
Wabunge hao, ambao kwa sasa ni miongozi mwa watunga sheria wanaolipwa fedha nyingi barani Afrika, walitaka kupatiwa kitika hicho cha fedha pindi bunge litakapovunjwa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mnamo Machi 2013.
Hata hivyo hoja yao hiyo ya kutaka kulipwa fedha hizo imezua maandamano ya kuipinga yanayosema wana tamaa kama ya fisi.
Rais Kibaki amesema posho hizo ni kinyume na katiba na zike nje ya uwezo wa serikali ukizingatia hali halisi ya nchi hiyo kifedha.
Wabunge hao 222 wa Kenya wanapokea mshahara usiokatwa kodi unaofikia takriban dola za marekani elfu 10 kwa mwezi.