RUFAA
ya kupinga kuvuliwa ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (CHADEMA), inatarajiwa kusikilizwa kesho na jopo la majaji
watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mohamed Chande.
Majaji wengine waliopo katika kusikiliza rufaa hiyo inayovuta hisia za
watu wengi ni pamoja na Jaji Natalia Kimaro na Salum Massati, wote wa
Mahakama ya Rufaa nchini.
Rufaa hiyo ambayo ilipaswa kusikilizwa Septemba 23, mwaka huu,
ilisogezwa mbele hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili wa pande zote mbili
kupatwa na dharura, ambapo jopo hilo liliridhika na hivyo kusogeza
mbele tarehe.
Jopo hilo lilizingatia barua iliyoomba kusogezwa mbele kwa shauri hilo
hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili, Tundu Lissu, anayemtetea Lema na
kaka yake, Alute Mughwai, anayewatetea walalamikaji kufiwa na baba yao
mzazi.
Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA),
anashirikiana na Wakili Mwandamizi Method Kimomogoro katika kumtetea
mrufani, Godbless Lema.
Kwa upande wake Wakili Mughwai anashirikiana na Wakili Modest Akida
kuwawakilisha wadaiwa katika shauri hilo ambao ni wanachama watatu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo.
Wanachama hao walifungua shauri lililotengua ubunge wa Lema wakidai kuwa
wakati wa kampeni alimdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda
Burian, kwa kutumia lugha za matusi.
Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, anayesaidiana na
Lissu, aliwasilisha katika mahakama hiyo hoja 18 za madai, akipinga
ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka
huu.
Katika baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua
uamuzi wa Mahakama Kuu, huku akiitaka mahakama hiyo imtangaze kuwa
mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika
shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na gharama za kesi
iliyomalizika katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila,
aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya
uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
No comments:
Post a Comment