|
Edward Christopher kushoto akimpongeza Kiemba aliyepiga mbili leo |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC
imezidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia
ushindi wa mabao 4-1 ilioupata jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji
wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa
kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa
Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele
kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba
katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya
29.
Kiemba
alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati
bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na
mashambulizi ya upande wa kulia.
Ilikuwa
rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na
mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
Nonga naye
alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha
wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni
kiulaini.
Bao hilo
lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia
mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
Kipindi cha
pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo
liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu
kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao
mawili zaidi.
Dakika ya 83
Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya
muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea
kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru penalti
sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango huyo.
Awali ya
hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye
alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja
alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao
la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea
kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi
tano.
Simba SC;
Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema/Kiggi Makassy, Shomary
Kapombe, Juma Nyosso, Amri Kiemba, Jonas Mkude/Daniel Akuffo, Mwinyi Kazimoto,
Felix Sunzu, Edward Christopher/Haruna Moshi na Emmanuel Okwi.
JKT Oljoro;
Shaibu Issa, Yussuf Nachogote, Nafo Zuberi/Jackson Semfukwe, Salim Mbonde,
Marcus Raphael (Nahodha), Emanuel Memba, Karage Gunda, Saleh Iddi/Amir Omar,
Paul Nonga, Meshack Nyambele na Sixbert Mohamed/Essau Sanu.
|
Wachezaji wa Simba |
|
JKT Oljoro wakiomba dua |
|
Kipa wa Oljoro, Shaibu Issa akidaka mbele ya Edward Christopher |
|
Edward Christopher kulia akimnyatia kipa wa Oljoro, Shaibu Issa |
|
Edward Christopher akichanja mbuga |
|
Emanuel Okwi akipasua msitu wa mabeki |
|
Edward Chiristopher akisafiri |
|
Simba wakishangilia |
|
Kiemba anafunga |
|
Kiemba anashangilia |
|
Mkude anampogeza Kiemba |
|
Kikosi cha JKT Oljoro leo |
|
Juma Nyosso |
|
Kocha wea Oljoro, Mbwana Makatta |
|
Jonas Mkude |
|
Kikosi cha Simba leo |
No comments:
Post a Comment