Pages

Friday, November 9, 2012

Lema Aponea Chupuchupu...!




RUFAA ya aliyekuwa Mbunge  wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema imeponea chupuchupu kutupiliwa mbali baada ya Mahakama ya Rufani, kukubali hoja moja ya pingamizi la makada wa CCM dhidi ya rufaa hiyo.

Mahakama hiyo ilikubali hoja ya wajibu rufaa kuwa rufaa hiyo ilikuwa  na dosari kutokana na tofauti ya vifungu vya sheria vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge na vilivyotumika katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na rufaa hiyo.

Hata hivyo, kilichomwokoa Lema ni kifungu cha 111 cha Kanuni za Mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya kanuni hiyo dosari hizo zinaweza kurekebishwa.

Chini ya kanuni hiyo, Mahakama ya Rufani ilimwamuru Lema kupitia kwa mawakili wake, Tundu Lissu na Method Kimomogoro, kufanya marekebisho ya dosari hizo zilizobainika na kisha kuwasilisha upya rufaa yake ndani ya siku 14 kutoka jana.

Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, 2012 kutokana na kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu  wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Lakini baadaye alikata rufaa Mahakama ya Rufani, kupitia kwa wakili wake, Method Kimomogoro kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, huku akitoa hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.

Tarehe ambayo rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la  majaji watatu Mahakama ya Rufani; Salum Massati, Natalia Kimaro  na  Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande (kiongozi wa jopo), wakili wa wajibu rufaa, Alute Mughwai, aliweka pingamizi la awali.

Katika pingamizi hilo,wakili Mghwai aliiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo, akidai kuwa ina kasoro za kisheria na za kikanuni huku akibainisha hoja tatu za kuunga mkono pingamizi hilo.

Hoja hizo za pingamizi la awali zilikuwa ni pamoja na kuchanganywa au kutofautiana kwa vifungu vya Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 2010, kati ya hukumu iliyomvua ubunge na hati ya kukaza hukumu hiyo.

Pia hoja nyingine ni kwamba hati ya kukaza hukumu hiyo haikuwa na mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe ambayo  hati hiyo ya kukaza hukumu ilitolewa.

Hoja ya tatu ilikuwa ni mtindo wa kuandika hati ya kukaza hukumu, kwa kutokuandika maneno, “imetolewa kwa mkono wangu na mhuri wa mahakama.”

Hata hivyo, katika uamuzi wake jana, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja moja ya pingamizi hilo, kuwa tofauti au kuchanganywa kwa vifungu hivyo vya sheria ni dosari ambayo inaifanya hati hiyo isiwe halali na ikatupilia mbali hoja nyingine mbili kuwa hazina msingi.

Uamuzi huo ulioandikwa na Jaji Nathalie Kimaro kwa niaba ya jopo hilo, ulisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma.

No comments:

Post a Comment