Pages

Tuesday, November 6, 2012

MAFUTA YAPO, MAGARI YANAENDELEA KUJAZA KAMA KAWAIDA ILI YAWEZE KUSAFIRISHWA KWENYE MIKOA TOFAUTI NCHINI, JAMBO AMBALO TUNAAMINI LINAWEZA KUPUNGUZA MALALAMIKO KWA WANANCHI,”- EWURA


Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Haruna Masebo
--
Patricia Kimelemeta  na Nuzulack Dausen
LICHA ya baadhi ya  mikoa kuendelea kulalamikia uhaba wa mafuta katika baadhi ya vituo,Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imesisitiza kuwa, mafuta yapo, na kwamba wanaoshindwa kuuza wana sababu zao.

Mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Mbeya, Singida na Tanga ambapo baadhi ya wananchi wameendelea kulalamikia kukosa huduma hiyo, jambo ambalo limesababisha kupanda kwa gharama za usafiri.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alisema kukosekana kwa nishati hiyo kwenye maeneo hayo kunatokana na umbali uliopo,lakini mafuta yapo, na kwamba magari yameendelea kujaza ili waweze kuyasambaza mikoani.

Alisema kutokana na hali hiyo wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuwa na subira kwa sababu tayari mafuta yamepelekwa kwenye mikoa hiyo, jambo ambalo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo.

“Mafuta yapo, magari yanaendelea kujaza kama kawaida ili yaweze kusafirishwa kwenye mikoa tofauti nchini, jambo ambalo tunaamini linaweza kupunguza malalamiko kwa wananchi,”alisema Kaguo.

Aliongeza ili kuthibitisha suala hilo,ripoti ya Novemba 3 mwaka huu inaonyesha kuwa, lita 141,000 za petroli na lita 168,000 za dizeli zilipelekwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kusambaza kwenye vituo vya mafuta na kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema magari hayo pia yalijaza lita 15,000 za petroli na lita 39,000 za dizeli ambazo zilipelekwa mkoani Singida kwa ajili ya kuwauzia wananchi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa uhaba wa mafuta katika mikoa hiyo ni mdogo ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Alisema kampuni za mafuta zilichukua lita 19,000 za petroli na lita 53,000 za dizeli kwa ajili ya Mkoa wa Tanga, licha ya kuonekana kuna upungufu wa mafuta ya taa.

Alisema  kutokana na hali hiyo tatizo la uhaba wa mafuta linaendelea kupungua siku hadi siku, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, tayari Serikali imeanza kudhibiti hali hiyo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo muhimu.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ewura iliomba kibali cha kununua mafuta yaliyotakiwa kuuzwa nje ya nchi ambayo ni zaidi ya lita21.24 milioni za petrol ambazo zitatosheleza kwa siku 12,wakati mafuta ya dizeli lita 35 milioni ambayo yanaweza kutosheleza kwa siku 17,mafuta ya ndege lita 11.17 milioni za mahitaji ya siku 25 na mafuta ya taa lita 1.5 milioni ambayo yatatosheleza kwa siku saba.

Hata hivyo, kuna meli zitakazoleta mafuta kuanzia Novemba 3 hadi 5 mwaka huu zenye tani za ujazo 32 milioni za mafuta,wakati tani za ujazo 23 milioni za dizeli na tani za ujazo 14 milioni za petroli zinatarajiwa kuingia kuanzia Novemba 10 hadi 12 mwaka huu.

Mwisho

No comments:

Post a Comment