Pages

Saturday, November 10, 2012

Mapya Yaibuka Mauaji Ya Profesa Mwaikusa



Profesa Juan Mwaikusa

MIAKA zaidi ya miwili sasa tangu Profesa Juan Mwaikusa auawe katika mazingira ya kutatanisha nyumbani kwake eneo la Salasala, Dar es Salaam, si familia yake wala umma wenye kuelewa kinachoendelea, wote wako gizani kuhusu wauaji wa gwiji huyo wa sheria. 

Ndugu kwa upande wao, hususan mke wake, wamekuwa wakifuatilia hatma ya kesi kuhusu watuhumiwa wa mauaji hayo, lakini juhudi zao hazijaweza kuzaa matunda, kesi bado iko katika hatua za awali kabisa, bado haijafikishwa Mahakama Kuu, kikubwa wanachoambulia ni kuelezwa kuwa kesi hiyo si nyepesi kama inavyoonekana kwa juu juu, bali ni ngumu ikiwa na mlolongo wa watu waliojificha katika kivuli cha watuhumiwa waliokamatwa.

“Sifahamu lolote linaloendelea babangu, kila ninapofuatilia polisi na mahakamani, naambiwa wanaendelea na uchunguzi. Baadhi ya wanafunzi wake walinisaidia kuandikia barua kwenda Kisutu, lakini nako nilielezwa upelelezi bado, wanasema kesi ni ngumu sana, inaonekana kuna watu zaidi ya wale waliokamatwa,” anasema Rhopea Mwaikusa, mjane wa marehemu Profesa Mwaikusa katika mahojiano na Raia Mwema.

Profesa Mwaikusa alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria. Aliuawa na watu wasiojulikana usiku wa Julai 13, mwaka 2010 wakati akirejea nyumbani.
Mengi yamezungumzwa kuhusu mauaji ya gwiji huyo wa sheria nchini, kila kundi likiibuka na nadharia yake kuhusu wahusika wa mauaji hayo, baadhi wakiyahusisha na kesi za watuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda aliokuwa akiwatetea katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda Jijini Arusha.

Wapo pia waliohusisha mauaji hayo na kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Balali, hao ni walioamini kuwa Gavana huyo alipata kukutana na Profesa Mwaikusa na inawezekana kuwa walizungumza kuhusu kashfa za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).


Hayo yakiendelea, sasa taarifa za kichunguzi ambazo Raia Mwema imefanikiwa kuzipata, zimeongeza utata zaidi katika sababu za mauaji hayo, zikieleza kwamba mauaji ya Profesa Mwaikusa yanaweza kuwa yalifanywa kwa maelekezo ya baadhi ya watawa wa Shirika la Wabenedikti wa Peramiho, wafanyabiashara, wahalifu na viongozi ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma.
Habari zaidi zinasema wahusika kwa mujibu wa taarifa hizo mpya, wamekuwa wakijichimbia Peramiho, Songea, mkoani Ruvuma na Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mauaji ya Profesa Mwaikusa yalipangwa na kuratibiwa ndani ya Shirika la Watawa la Peramiho mkoani Ruvuma ambako inaelezwa ndimo walimo wahusika wakuu wa mauaji hayo kutokana na ugomvi wa umiliki wa mgodi wa dhahabu wa Lukarasi ulioko wilayani Mbinga, uliokuwa unamilikiwa na Shirika la Benedikti la Peramiho.

Taarifa zinasema kwamba Profesa Mwaikusa alikuwa akihifadhi nyaraka za umiliki wa mgodi huo na yalikuwapo maagizo kutoka kwa mkubwa wa Shirika, anayetajwa kwa jina la Fr. Lambert, akiwaagiza wakurugenzi walioteuliwa kusimamia hisa za shirika hilo kwenye mgodi huo kutofanya jambo lolote pasipo kumshirikisha Profesa Mwaikusa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Profesa Mwaikusa naye alikuwa ameteuliwa kuwa mmoja wa wawakilishi wa shirika hilo kwenye mgodi huo wa dhahabu, kwa barua ya Agosti 12, 2003 iliyowekwa sahihi na Buruda Aidan na Buruda Edmund wote wakionyeshwa kuwa na hisa 2000.
Wawakilishi hao wawili waliteuliwa na Mkubwa wa Jumuiya hiyo ya watawa wa Peramiho wakiwa watawa na kuongezewa mtu mwingine, mkazi mmoja wa Songea Mjini anayetajwa kwa jina la Steven Haule ambaye hakuwa mtawa.

Uteuzi wa wawakilishi hao uliibua uhasama mkubwa miongoni mwa watawa wenzao likiibuka kundi la watawa waliotaka wakabidhiwe jukumu la kuwakilisha shirika hilo huko mgodini. Inaelezwa kuwa ni kundi hili lililopanga njama za kupora nyaraka hizo kwa gharama yoyote hata ikiwa ni kutoa uhai wa wawakilishi halali wa shirika hilo.

Taarifa zinasema akiwa mwakilishi wa Shirika la watawa hao, Profesa Mwaikusa alisimamia sheria akiwataka watawa hao kufuata sheria katika kuuchukua mgodi huo wa Lukarasi, msimamo ambao hawakukubaliana nao kutokana na mazingira ya usiri katika umiliki wa mgodi wenyewe, usiri uliowanufaisha zaidi watawa hao.

Vielelezo mbalimbali, ambavyo Raia Mwema imefanikiwa kuvipata, vinawaonyesha baadhi ya viongozi wa zamani wa shirika hilo kuwa nyuma ya kundi hilo la watawa na washirika wao waliopanga mipango ya kupora nyaraka hizo za siri kutoka kwa Profesa Mwaikusa, na wanatajwa kuanzisha uhasama mkubwa na viongozi wapya walioteuliwa na aliyekuwa Mkubwa wa Shirika hilo la Peramiho, Fr. Lambert.

Siri katika umiliki wa Mgodi wa Lukarasi

Nyaraka zinaonyesha kuwa shirika hilo linamiliki mali mbalimbali zikiwamo nyumba, magari, bunduki, viwanja na mgodi wa dhahabu wa Lukarasi huko Mbinga mkoani Ruvuma.
Hata hivyo, nyaraka hizo zinaonyesha kuwa shirika hilo limekuwa likimiliki mgodi huo kwa siri ambapo hutumia wawakilishi wanaojitokeza kwenye nyaraka za shirika hilo.

Shirika hilo la watawa wa Peramiho, lilinunua hisa kwenye Kampuni ya UMICO, inayomiliki mgodi huo wa dhahabu wa Lukarasi, kwa dola zinazoelezwa kuwa zaidi ya laki tatu, na vyanzo ndani ya Shirika hilo la “Roman Catholic Benedict’s Abbey of Peramiho” vinabaisha kuwa lilitoa shilingi bilioni mbili na kusimamia uendeshaji wa mgodi huo kwa siri.

Kwa mujibu wa nyaraka za kampuni hiyo kwa mwaka 1997, wanahisa wa Kampuni ya UMICO, wanaonyeshwa kuwa ni Barnabas Mathew, Dismas Ndunguru, Johnson Nchimbi, Francis Kayombo, Kenneth Nchimbi na Karim Hassanali Teja Kanji.

Hisa za shirika hilo kwenye ndani ya UMICO hazikuandikwa kwa jina la Peramiho. Hata hivyo, kumbukumbu za kununua hisa zinalifichua shirika hilo pale zinapoonyesha kuwa Peramiho ni mwanahisa ambazo ameaminishwa Johnson Nchimbi, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UMICO Ltd azishikilie kwa niaba ya shirika.

Miongoni mwa nyaraka hizo, ni zile za ununuzi wa hisa kutoka kwa mwanahisa Karim Kanji, mawasiliano ya shirika na Kanji kuhusu malipo ya hisa hizo na nyaraka za kisheria kuhusu uteuzi wa wawakilishi wa shirika hilo katika Kampuni ya UMICO, na kila mmoja alisaini nyaraka zake pamoja na mwanasheria wao, Profesa Mwaikusa, Juni 17, 2003.

Nyaraka hizo za uteuzi zilikuwa ni za pamoja na Buruda Mhuwa, Buruda Kimario na Haule, ambapo ni katika nyaraka hizo pia zinatajwa hisa 4,250 za shirika hilo kwenye mgodi wa Lukarasi, mgawanyo ukiwa wawakilishi watawa wawili hisa 2000 kila mmoja na Haule hisa 250.
Katika nyaraka hizo pia ndimo inamobainishwa ushiriki wa Nchimbi katika kulifichia siri shirika hilo hizo hisa 4250.
Utaratibu uliotumiwa na shirika hilo kumiliki mgodi huo wa dhahabu wa Lukarasi, ndio unaowapa nguvu watawa hao pamoja na washirika wao kuwaelekeza wachunguzi wa kadhia hii kwenda Brela wakifahamu fika kuwa kule shirika halipo, lakini wakati huo huo wakisahau kuwa kuna nyaraka nyingine zinazowahusisha moja kwa moja na umiliki wa mgodi huo.

“Sifahamu chochote, hatuhusiki na mgodi wa Lukarasi, I know nothing about it, nenda Brela upate members wa mgodi, sawa? bye,” alijibu Buruda Fidelis Mligo alipotakiwa kuelezea anachofahamu kuhusu mgodi huo.

Jibu la aina hiyo hiyo lilitolewa na Johnson Nchimbi katika mahojiano yake na Raia Mwema kwa simu akisema: “Mimi siko authorized (siruhusiwi) kutoa taarifa za kampuni. Ni vema ukaenda Brela.” Hata hivyo, baadaye alizungumza kuonyesha yamekuwepo mawasiliano na Buruda Mligo akisema: “ Jana Br (Buruda) Fidelis alipigiwa simu kutoka Raia Mwema, hakufurahishwa na maswali, nikamwambia wakikupigia tena waambie waende Brela.”

Nchimbi alisema tena baaaye: “Si vema mtu kukupa taarifa, mimi si msemaji wa kampuni, ukitaka taarifa zaidi tuwasiliane.”Vyanzo vya ndani ya shirika hilo vinaashiria kwamba mauaji ya Profesa Mwaikusa yana mkono wa baadhi ya watawa ndan i ya shirika hilo.

Aidha, taarifa nyingine zinamtaja mtu ambaye alikuwa karibu kabisa na Profesa Mwaikusa kusaidia kufanikisha mpango huo kama Profesa Mwaikusa asingekubali kutoa nyaraka za shirika.
Vyanzo ndani ya familia ya marehemu pamoja na taarifa za maandishi zinaibua mazingira ya mashaka kuhusu mahusiano ya mtu huyo na marehemu, siku chache kuelekea mauaji hayo. Familia ya marehemu Mwaikusa inathibitisha kupotea kwa mtu huyo tangu ilipohamia Salasala kutoka Kunduchi jambo lililowashangaza kwani haikuwa kawaida yake.

Maelezo hayo yanaoana na ya vyanzo ndani ya shirika hilo vinavyoeleza kuwa marehemu akiwa na mkurugenzi mmoja wa watawa waliokuwa wakisimamia mgodi huo, walikubaliana na mtu huyo wakutane nyumbani kuzungumzia ujumbe uliokuwapo kuhusu kundi la watawa waliotaka kuchukua mgodi kwa nguvu, lakini katika hali iliyowashangaza, rafiki huyo wa marehemu hakufika na hawakuonana naye tena hadi Profesa Mwaikusa anauawa.

Taarifa zinasema wakati wa msiba mtu huyo alifika nyumbani kwa marehemu eneo la Salasala, ikiwa ndiyo mara yake ya kwanza tangu familia hiyo ihamie huko.Mawasiliano ya watawa hao na Profesa Mwaikusa kabla ya mauaji yake, vinaonyesha kuwa mbali ya yeye, kulikuwa na watu wengine watatu zaidi waliokuwa kwenye orodha ya kuuawa, na kwamba tayari walishahisi kuwapo kwa njama hizo. 

Profesa Mwaikusa alikuwa mhimili mkuu wa Kampuni ya UMICO na mmoja wa wawakilishi wa Shirika ndani ya UMICO. Baada ya mauaji yake, wakurugenzi waliobaki nao walijikuta katika wakati mgumu, wakilazimishwa kuachia nafasi zao.

Chanzo: http://www.raiamwema.co.tz/mapya-yaibuka-mauaji-ya-profesa-mwaikusa

No comments:

Post a Comment