Pages

Tuesday, November 6, 2012

Pigo kubwa Chadema Madiwani, Mkurugenzi, Makatibu Wakutwa na hatia



 
Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Mwanza imewatia hatiani viongozi watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwamo madiwani wawili kwa kosa la kukaidi amri ya Mahakama.
Viongozi waliotiwa hatiani ni madiwani Dan Kahungu wa Kata ya Kirumba na Josephat Manyerere wa Kata ya Nyakato ambaye kabla ya kuondolewa kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye alikuwa ndiye Meya wa Jiji la Mwanza.
Viongozi wengine wa Chadema waliotiwa hatiani na Mahakama hiyo ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema Taifa, Benson Kigaila, Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, John Anajus na Katibu Mwenezi wa wilaya hiyo, Carlos Majura.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Angelo Rumisha, ndiye aliyewatia hatiani viongozi hao, lakini hakutamka adhabu watakayotumikia kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kutokana na baadhi ya watuhumiwa kutokuwepo mahakamani hapo.
Diwani Kahungu na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Anajus ndio waliokuwepo mahakamani wakati Hakimu Rumisha akitangaza kuwatia hatiani na aliamuru wapelekwe rumande hadi wenzao watatu watakapokamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mbali na kuwatia hatiani viongozi hao wa Chadema, Hakimu Rumisha alisema kwamba maamuzi ya awali yaliyotolewa na Mahakama ya kutengua hatua ya Matata na mwenzake kuvuliwa uanachama yatabaki kama yalivyo hadi itakapoamuliwa vinginevyo katika kesi ya msingi.
Hatua hiyo ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi jijini Mwanza kuwatia hatiani viongozi hao wa Chadema, inafuatia tukio la Kamati Kuu ya Chadema kuwavua uanachama madiwani Henry Matata wa Kata ya Kitangiri na Adam Chagulani wa Kata ya Igoma.
Baada ya madiwani hao kuvuliwa uanachana, Matata alifungua kesi ya kupinga hatua hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi jijini Mwanza ilitoa amri ya kutaka madiwani hao wasizuiwe kuendelea na shughuli zao na watambuliwe kama wanachama halali wa Chadema
Hata hivyo, Septemba 25, mwaka huu, Chadema Wilaya ya Ilemela kilifanya mkutano wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Meya na Naibu Meya wa manispaa hiyo, hatua ambayo inaonekana kuwa sababu ya Diwani Matata kuamua kufungua kesi dhidi ya baadhi ya washiriki wa mkutano huo akiwamo Kigaila (Mkurugenzi wa Oganaizesheni) akiwatuhumu kukiuka amri ya Mahakama kwa kutomshirikisha.
Oktoba 13 mwaka huu baadhi ya magazeti yalichapisha habari kuhusiana na malalamiko ya Chadema Wilaya ya Ilemela kwamba zipo njama zinazomhusisha Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Angelo Rumisha, za kutaka kukihujumu chama hicho katika uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela.
Chama hicho kilidai kwamba hujuma hiyo inalenga kutaka kuwahukumu kifungo cha miezi sita jela madiwani wake wawili ili wasipate fursa ya kushiriki uchaguzi wa Meya na Naibu wake unaotarajiwa kufanyika hapo baadaye baada ya kuahirishwa katika mazingira ya kutatanisha.
Kufuatia kuwepo kwa tetesi hizo, Chadema kiliamua kumuandikia barua Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kumtaka aingilie kati suala hilo na kuhakikisha haki inatendeka.
Katika barua hiyo yenye Kumbukumbu Namba CDM/w.IL/2012/01 ya tarehe 11/10/2012 ambayo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Yunus Chilongozi, kwenda kwa Jaji Mfawidhi, chama hicho kilidai kwamba Madiwani wanaolengwa katika mpango huo ni Dan Kahungu wa Kata ya Kirumba na Josephat Manyerere wa Kata ya Nyakato.
Mbali na madiwani hao, barua hiyo iliwataja watu wengine wanaolengwa katika njama hizo kuwa ni Kigaila, Anajus, Majura na Baraza la Wadhamini la chama hicho.
Chadema kimedai katika barua yake hiyo kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Mwanza imeamua kukubali maombi yenye lengo la kutaka kuwatia hatiani viongozi hao kama wafungwa wa kimadai (civil prisoners) kwa kosa la kutotii amri ya Mahakama.
“Mheshimiwa jaji Mfawidhi, maombi hayo yaliyowasilishwa na Henry Mtinda Matata kupitia mawakili wake, Magongo na Matata, yakasajiliwa kama Misc.
Application No.66/2012 yanaonekana yamelenga hasa madiwani hao wawili kama njia ya kuwakomoa na kuwasababishia kukosa nafasi ya kushiriki uchaguzi wa umeya wa Manispaa mpya ya Ilemela,” inasema sehemu ya barua hiyo.

No comments:

Post a Comment