Pages

Tuesday, November 6, 2012

SIMBA WAANZA KUWEWESEKA BAADA YA KUTANDIKTWA BAO 2-0 DHIDI YA MTIBWA SUGAR LIGI KUU YA VODACOM MJI KASORO BAHARI.




Nahodha wa klabu ya Simba Juma Kaseja akibubujikwa na machozi huku Daniel Akuffo akimsihi aliendelee kulia baada ya klabu yake kutandikwa bao 2-0 na Mtibwa Suagar ya Manungu Turiani Morogoro katika mchezo wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara juzi uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.


MPASUKO, mgawanyiko, msambaratiko hayo ni baadhi ya maneno unayoweza kuyatumia katika kuelezea hali ya sasa iliyoizunguka klabu ya Simba.


Mabingwa hao watetezi mwishoni mwa wiki iliyopita walipoteza uongozi wao wa Ligi Kuu kwa watani zao Yanga baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.


Kabla ya kipigo hicho cha Jumapili, Simba tayari ilishatoa sare mara tano mfululizo dhidi ya Yanga 1-1, Coastal Union, Mgambo Shooting 0-0, Kagera Sugar 2-2 na Polisi Moro 1-1 matokeo yaliyosababisha uongozi wake kumsimamisha Haruna Moshi na kumpeleka timu ya vijana beki Juma Nyoso.


Katika mechi ya Simba dhidi ya Mtibwa, wakati wa mapumziko kipa Juma Kaseja na mshambuliaji Emmanuel Okwi walitaka kupigana kabla ya kuamuliwa, lakini hiyo yote ilitokana na Mganda huyo kumlaumu Kaseja kuwa ndiyo chanzo cha kusababisha Simba kufungwa na Mtibwa kwa kusababisha bao la kwanza.


Bao lililozua tafrani hiyo lilikuwa ambalo Kaseja alipangua shuti la Vincent Barbanas na mpira kumkuta mshambuliaji Mohamed Mkopi aliyeukwamisha wavuni mpira huo kirahisi.


Hata hivyo habari ambazo Mwananchi limezipata baada ya mechi hiyo ya Simba dhidi ya Mtibwa zinadai sababu kubwa ya Simba kufanya vibaya ni kutokana na ushindani uliopo kati ya Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope.


"Wachezaji na viongozi wa Simba wamegawanyika kwenye makundi mawili kuna wale waliokuwa upande wa Kaburu na wale ambao wapo kwa kundi la Friends of Simba linaloongozwa na Hanspope," kilidai chanzo hicho.


Chanzo hicho cha habari kilisema,"uhasama kati ya pande hizi mbili ulianza baada ya Kaburu kukubali Kelvin Yondani auzwe Yanga pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wa kigeni ambao wengi walikuwa mzigo kwa Simba hali iliyosababisha Kaburu kunyang'anywa mamlaka ya kusajili wachezaji na Hanspope kuchukua jukumu hilo."


Chanzo hicho cha habari kinadai kuwa baada ya Hanspope kuchukua jukumu la kusajili wachezaji alisajili, ambapo anataka wachezaji wake wapangwe kwenye mechi na Kaburu anataka wachezaji wake wapangwe hali inayofanya hiongozi hao watofautiane na timu ifanye vibaya.


Akilizungumzia sakata hilo, Hanspope ambaye pia ni Mwenyekiti wa ëFriends of Simbaíaliyechaguliwa Agosti 24, alisema,"sina tofauti yoyote na Kaburu, mimi ni mwenyekiti wa kamati ya usajili yeye ni makamu mwenyekiti, hatuingiliani kabisa katika mgawanyo wa kazi zetu sasa tutofautine kwa lipi?."


Alisema,"wanachosema wanachama ni hisia tu hakuna tofauti yoyote na hata kama tuna tofauti inahusiana nini na matokeo?, ninachowaomba watulie tumalize mzunguko wa kwanza salama tuangalie wapi tulipokosea tujipange upya."


Hanspope alisema, "matokeo mabovu ni suala la kiufundi zaidi na kocha ndiyo anahusika kupanga wachezaji ambao hawana viwango, ukimshauri wachezaji wa kupanga yeye hafuati ushauri anaamua anavyojua yeye matokeo yake ndiyo haya.


Akimzungumzia mshambuliaji Daniel Akuffo, Hanspope alisema,"Akuffo ukiniuliza anafanya nini mimi sijui, hafungi magoli, ukimwambia mwalimu yupo Edward Christopher mpange, yeye anamng'ang'ania Akuffo wake hilo ndiyo tatizo."


Aidha Hanspope alisema,ìFriends of Simba, tunachokifanya lazima kiendane na tafsiri ya neno lenyewe na isije ikawa tofauti, kuwa ni maadui wa Simba, naomba ushirikiano wa pamoja wa wanasimba kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu.î


Naye Kaburu akilizungumzia sakata hilo alisema hana matatizo yoyote na Hanspope na watu wanaosema hivyo hawajui lolote kwani wao ni viongozi wawili wenye majukumu tofauti.


"Simba haiongozwi na mtu mmoja ina mwenyekiti na mimi ni msaidizi wake, kuna kamati ya usajili, mashindano, ufundi, kila mtu anatekeleza wajibu wake, kutofanya vizuri kwenye timu kama viongozi tunasikitika, kufukuzana siyo dawa na wala hatujengi,  tunatakiwa kukaa chini na kuangalia ni wapi tumekosea tujirekebishe,"alisema Kaburu.


Alisema,"ninachoona ni tatizo la ufundi, mwalimu alitakiwa kubuni fomeshini ya kukabiliana na viwanja vibovu, kushutumu wachezaji wamechukua rushwa au viongozi wanahujumu timu siyo kitu kizuri ni kitu kibaya sana, kwani wachezaji hawa hawa na mwalimu huyu huyu ndiyo waliochukua ubingwa mwaka jana, pia mwaka huu wamechukua mataji manne tofauti tofauti."


WANACHAMA WAVAMIA KLABUNI


Baadhi ya wanachama wa Simba jana walifanya maandamano makubwa makao makuu ya klabu hiyo kwenye mtaa wa Msimbazi kushinikiza viongozi wao wajiuzulu kwa madai kuwa wameshindwa kuongoza timu.


Wanachama hao walikuwa na mabango yaliyobeba ujumbe tofauti tofauti ukiwashutumu Rage, Kaburu na Kaseja waachie ngazi kwa kile walichodai kuwa wanahujumu timu yao.


Baadhi ya mabango hayo yalisomeka,"Mheshimiwa Rage una kazi nyingi tuachie Simba yetu...."Wachezaji acheni kuidhalilisha Simba kwa pesa za mafisadi ...."Kocha wetu Milovan bado tunamuhitaji mchango wake mkubwa...."Kaburu ulitaka kumuuza Okwi sasa unamtumia kuhujumu...."Kaburu, Kaseja achieni ngazi.....".


Akizungumza kwa hisia mwanachama Said Moscow kadi namba 250 alisema huku akishangiliwa na kundi kubwa la wanachama,"viongozi ndiyo wanachangia matokeo mabovu, wenyewe kwa wenyewe hawaelewani, wanaweka matabaka kwa wachezaji, wameshindwa kuongoza timu, bora waachie ngazi."


"Kaburu asikwepe lawama za matokeo mabovu yeye ni kiongozi amekuwa akiuza wachezaji,  Kaseja naye ana dhambi zake umri umeenda, kiwango kimeshuka bado anang'ang'ania anang'ang'ania kitu gani?, Kaseja kachoka atafutwe kipa mwingine, tutafanya mkutano wa wanachama kwa mujibu wa katiba yetu wanachama 500 tunataka viongozi wajiuzulu,"alisema Moscow.


Naye mwanachama Mgeni Ramadhani maarufu kwa jina la 'Macho' aliongea kwa hasira akisema," Yondani kauzwa Yanga, Okwi naye alitaka kuuzwa Yanga, Kaburu ndiyo tatizo, Hayati mwalimu Nyerere alisema kiongozi anayeingia madarakani kwa fedha huyo hatufai."


Alisema,"tunampa siku mbili atangaze kwa hiyari yake kujiuzulu la sivyo tutaandamana mpaka nyumbani kwake Mbezi anapoishi tunapajua."


Akizungumzia suala la mashabiki kuandamana hadi nyumbani kwake kushinikiza ajiuzulu, Kaburu alisema,"ninachowaomba wanachama watulie katika kipindi hiki, wasubiri tumalize mchezo wetu wa mwisho na Toto, kuna likizo ndefu tutakaa na kuangalia cha kufanya, kuandamana hadi nyumbani kwangu siyo dawa, atakayefanya hivyo nitamchukulia kama mhalifu na nitamchukulia hatua, kufungwa mechi moja siyo tatizo, Yanga wamepoteza mechi mbili mbona hawajaandamana?, kuna watu wana chokochoko walikuwa wanasubiri timu ifanye vibaya wapate cha kusema."

No comments:

Post a Comment