Pages

Saturday, December 15, 2012

Apendekeza Wabunge Kuchapwa Viboko



 Na: Matern Kayera, Kinondoni
                                                                                       
MKAZI wa Kata ya Makuburi Wilaya ya Kinondoni, Pendo Mlyauke (35) jana alipendekeza adhabu ya viboko isiishie shuleni tu bali ifike hadi bungeni. Alisema kuwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu bungeni, Katiba Mpya haina budi kuja na sheria itakayo ruhusu adhabu ya viboko kwa wabunge wasio na maadili.

Pendo aliyasema hayo wakati akiwasilisha maoni yake ya kuundwa kwa Katiba Mpya mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Alisema kuwa kitendo cha wabunge kuwa huru bila utendaji wao kufuatiliwa na kuhojiwa ndiyo sababu inayochangia wengi wao kukosa nidhamu wawapo bungeni.

“Siku hizi Bunge limekuwa kama uwanja wa malumbano. Utawakuta wanasema na kujibizana ovyo ovyo, wengine wanalala muda wote wakati Bunge linaendelea, napendekeza kuwepo adhabu ya viboko kwa wabunge wa aina hiyo kwani wanayoyafanya ni kinyume cha maadili,” alisema Pendo.

Aliongeza kuwa kama nchi za Rwanda na Burundi wabunge wasiokuwa na maadili wanaadhibiwa, inakuwaje hapa nchini wanaachwa huru. Alisema kuwa ili kukomesha utovu huu wa nidhamu kwa wabunge, Katiba Mpya inapaswa kutoa adhabu kali ya viboko visivyopungua 4 na adhabu hiyo akapendekeza itolewe na wanajeshi.

Kuhusu wanafunzi, alisema kuwa hivi sasa kuna tatizo kubwa la nidhamu kwa wanafunzi shuleni kutokana na adhabu ya viboko kuondolewa. Alipendekeza adhabu hiyo irudishwe mashuleni na ikiwezekana kila mwalimu awe na uwezo wa kuchapa kama ilivyo zamani.

Naye Thomas Muhahate (63) alipendekeza kuwa maneno yanayosemeka katika Katiba iliyopo kuwa kila mtu na haki ya kumiliki mali yana upungufu, hivyo akapendekeza kwenye Katiba Mpya neno halali liongezwe. Alisema kwamba kama Katiba ikiendelea kuweka mwanya huu, matokeo yake ni kuongeza kundi la mafisadi wa mali za umma ambao mali walizonazo siyo halali.

“Mali za Watanzania zinahujumiwa kila siku, hii inatokana na Katiba iliyopo kusema kuwa kila mtu ana haki ya kumiliki mali. Mimi nasema Katiba Mpya itamke kuwa kila Mtanzania awe na haki ya kumiliki mali halali, ili mafisadi waweze kuhojiwa kama mali walizonazo ni halali na watoe uthibitisho,” alisema Muhahate.
Aliongeza kuwa vitendo vya ufisadi hapa nchini vimechangiwa na Azimio la Zanzibar lililofuta Azimio la Arusha. Alisema kuwa kufutwa kwa Azimio la Arusha kumechangia kuporomoka kwa maadili ya viongozi wa umma na matokeo yake wengi wamekuwa wakwapuaji wa mali za umma.

“Kumekuwa na wimbi la majumba kujengwa kama uyoga kila mahali. Haya ni matokeo ya ufisadi. Mbaya zaidi ni kwamba hakuna sheria ya kuwabana au kuwauliza wamepata wapi pesa za kujenga majumba hayo. Napendekeza Azimio la Arusha lirudishwe ili kujenga upya maadili ya viongozi wa umma na jamii,” alisema Muhahate

No comments:

Post a Comment