SIKU moja baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kutangaza kumsaka mtu aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa amevalia sare za jeshi hilo, chama hicho kimeibuka na kulijia juu jeshi hilo.Hata hivyo, mbali na kauli hiyo, jeshi hilo limekijibu Chadema likisema kwamba halifanyi siasa na kwamba litaendelea kumsaka mtu huyo, kwa kuwa kanuni zake haziruhusu askari kushabikia siasa.Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema chama hicho kimeshangazwa na kasi ya jeshi hilo kuchunguza tukio hilo, huku akidai kwamba kuna masuala mazito ambayo hayajatolewa ufafanuzi kama lile la Meremeta.“Serikali ilikataa kulifuatilia kwa madai ya kutokuingilia usiri wa jeshi hilo na halikutolewa ufafanuzi wala kufanyiwa uchunguzi mpaka sasa,” alisema Mnyika na kuendelea.
“Isitoshe Septemba, mwaka huu katika Mkutano Mkuu wa UVCCM Iramba, aliyekuwa Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho Mwigulu Nchemba (aliwahi kutoa matamko kuhusu JWTZ), lakini jeshi halikufikiria kuyatolea tamko.”
Mnyika alidai pia kuwa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, aliyekuwa Mnadhimu wa Jeshi hilo Luteni Jenerali Abdulahman Shimbo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuvitaka vyama vya siasa kutokugomea matokeo ya uchaguzi kwa madai ya kulinda amani ya nchi.
“Kauli ile ya Shimbo ni ya kisiasa na ya kibaguzi ambayo ililenga kuvididimiza vyama vingine na kuibeba CCM. Mbona jeshi halichunguzi kauli hiyo hata baada ya Shimbo kustaafu?” alihoji Mnyika.
Mnyika alisema kwamba Chadema hakitaki kutumia tukio hilo la askari kuhalalisha makosa mengine, bali inataka sasa JWTZ iwajibike kwa kila jambo linalolihusu badala ya kukimbilia masuala yaliyofanywa na askari wadogo.
Hata hivyo, Mnyika alisema chama hicho hakipo tayari kuingia katika mvutano na jeshi kuhusiana na tukio la askari huyo kujihusisha na siasa mpaka jeshi hilo litakapokamilisha uchunguzi na kutoa taarifa yake kwa umma.
Kwa upande wake, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa jeshi litaendelea kujiweka kando na shughuli za siasa na kusisitiza kuwa mtumishi wake yeyote anayetaka kujiingiza kwenye majukwaa ya kisasa anapaswa kujitoa jeshini.
Akijibu hoja za Chadema kuhusiana na tamko lilitolewa na aliyekuwa Mnadhimu wa jeshi hilo Shimbo aliyewataka wanasiasa kutogomea matokeo wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Mgawe alisema: “Ebwa ehh! Na wewe sasa unataka kuniingiza kwenye siasa, mimi sitaki kuingia huko, lakini nikueleze kuwa sisi kama wanajeshi tuko royal (utii) kwa Serikali iliyoko madarakani,” alisema Mgawe.
Alisema kwa mujibu wa sheria, Jeshi halipaswi kufungamana na itikadi zozote za kisiasa kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kulitumbukiza taifa kwenye hatari.
source gazeti la Mwanainchi
No comments:
Post a Comment