Pages

Wednesday, February 13, 2013

Walioshindwa kulipa mikopo BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), wafikishwa mahakamani .


 

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), imewafikisha mahakamani wanafunzi 18 waliochukua mkopo wa kuwawezesha kupata elimu ya juu na kushindwa kurejesha. Wanafunzi hao, wanadaiwa zaidi ya Sh milioni 148 ambazo walikopa kati ya mwaka 1994 na 2009 na kukubali kurejesha kwa muda ambao walikubaliana.

Katika hati ya madai iliyofunguliwa na bodi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, inadaiwa kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 6 C na H cha sheria ya Bodi ya Mikopo namba 9 ya mwaka 2004, inatamka kwamba bodi iliaminiwa kusimamia utaratibu mzima wa kutoa na urejeshaji wa mikopo iliyotolewa na Serikali tangu Julai 1994.

“Kwa mujibu wa kifungu namba 19 cha sheria ya bodi na miongozo yake, inatamka kila aliyefaidika na mkopo baada ya kukamilisha elimu yake, atarejesha mkopo wa Serikali kupitia Bodi.

“Wadaiwa walikumbushwa kurejesha madeni kupitia vyombo vya habari, lakini walikaa kimya hivyo bodi inaomba waamuliwe kulipa,” ilisema hati hiyo ya madai.

Bodi ya Mikopo, inaomba kila mdaiwa alipe fedha alizokopa na adhabu asilimia 10 ya mkopo, alipe fidia kama mahakama itakavyoona inafaa na pia walipe gharama za kesi.

Wadaiwa katika kesi hiyo, wanatakiwa kulipa jumla ya Sh 135,132,275 ambazo ni madeni waliyokopa kwa ajili ya kuwawezesha kupata elimu ya juu na Sh 13,513,227 ni fedha wanazotakiwa kulipa kwa adhabu ya kuchelewesha malipo.

Wanafunzi hao, waliofikishwa mahakamani ni Adam Coresh, Ally Mwenda, Anna Lymo, Hasma Tullango, Catherine Mhina, Clement Kihamia, Dorin Lyatuu, Farida Zuku na Felix Mosha.

Wengine ni Flora Peter, Frank Daniel, Harieth Mazengo, Happynes Saria, Hollo Ngeme, Mwanahamisi Abood, Ndebemeye Philipo, Ndeni Anande na Turphina Matereke.

Kesi hiyo ya madai, imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi na tarehe ya kuanza kusikilizwa itapangwa.

No comments:

Post a Comment