Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, March 11, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA SIMBA,SC




SALAAM,
JANA na leo, zimetolewa habari tofauti kuhusiana na kalbu ya Simba ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa taarifa hizo.

1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile anaidai Sh milioni 25 na anataka alipwe zote jana.
Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na wachezaji wote wa Simba katika hoteli hiyo usiku wa kuamkia jana.
Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi na walisubiri mpaka wakati timu inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua hiyo.
Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno. Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.
Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.
Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha hizo.
Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili kuongeza mapato yake. Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba nayo ifaidike.
Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu kigeni?
Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment