Pages

Wednesday, May 15, 2013

Diwani wa Chadema ashambulia Ng’ombe sita wa mpiga kura wake na kufyeka shamba la Alizeti Tazama picha



Baadhi ya Ng’ombe sita mali ya John Theodore Ghumpi wa kijiji cha Minyinga jimbo la Singida mashariki,waliokatwa katwa juzi na diwani wa CHADEMA kata ya Mungaa Matheo Alex kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ugomvi wa kugombea ekari 50 za mbuga.
Mkulima na mfugaji wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa jimbo la Singida Mashariki, John Theodore Ghumpi akionyesha Ng’ombe wake aliyekatwa kwa shoka na diwani wa kata ya Mungaa Matheo Alex kwa tuhuma ya kugombea mbuga ya ekari 50.

Kaimu OCD wilaya ya Ikungi, Deo Batete akiangalia kwa masikitiko Ng’ombe wa John Theodore Ghumpi aliyekatwa shoka na diwani wa kata ya Mungaa.Wa pili kushoto ni mkuu wa kituo kidogo cha polisi kata ya Mungaa  D/S/SGT Elibariki Urio.
Sehemu ya shamba la Alizeti mali ya mkulima John Theodore Ghumpi mkazi wa kijiji cha Minyinga linalodaiwa kufyekwa na diwani Matheo Alex.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa waliofika nyumbani kwa John Theodore Ghumpi ambaye Ng’ombe wake sita wanadaiwa kukatwa katwa kwa shoka na diwani Matheo Alex na vijana wake wawili .Pia diwani Matheo anadaiwa kufyeka shamba la Alizeti la ekari mbili na nusu.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
DIWANI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Mungaa jimbo la Singida Mashariki, Matheo Alex amewaacha midomo wazi wapiga kura wake na wananchi wa kata hiyo kwa kitendo chake cha kukata kata ng’ombe sita kwa shoka na kufyeka ekari mbili na nusu za shamba la Alizeti .
Imedaiwa kuwa diwani huyo kijana ametenda kitendo hicho ,kutokana na ugomvi wa kugombea mbuga ya ukumbwa wa ekari 50.
Ng’ombe hao waliokatwa katwa na diwani Matheo akishirikiana na watoto wake, watatu wana mimba, wawili wananyonyesha na moja ni dume wote ni mali ya John Theodore Ghumpi mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa. Ng’ombe hao na ekari la shamba la Alizeti lililofyekwa vyote vina thamani ya zaidi ya shilingi 4.5 milioni.
Tukio hilo la kusikitisha, limetokea mei 13 mwaka huu saa 5.00 asubuhi katika kijiji cha Minyinga jimbo la Singida Mashariki.
Diwani Matheo ambaye miaka miwili iliyopita aliwahi kushitakiwa katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida kwa kosa la kuvunja/kuharibu kwa makusudi kizuizi (geti) la kudhibti ushuru wa mazao ya misitu na kumpiga mlinzi wa geti hilo,anatuhumiwa pia kufyeka ekari mbili na nusu za shamba la Alizeti.
Akisimulia mkasa huo wa kusikitisha, Joseph Albino (mtoto wa kaka yake mkubwa na John mwenye ng’ombe zilizokatwa) amesema siku ya tukio alipita jirani na kaya ya diwani Matheo na kukuta diwani akiwa kwenye kikao na watu wasiopungua kumi.
Akifafanua, Albino amesema alipoonwa na diwani, diwani huyo aliwaamrisha waliokuwa kwenye kikao hicho,kuwa waanze kumuuwa yeye (Albino).
“Ghafla diwani Matheo na kundi lake walinyanyuka huku wakiwa wamebeba shoka, panga na hengo na kuanza kunifukuza,wakati wakiendelea kunifukuza njiani walikuta kundi la ng’ombe za John zikichungwa na ndipo walipoanza kuzikata kata wakiongozwa na diwani wetu”, amesema kwa masikitiko makubwa.
Naye mke wake John, Mary John amesema aliposikia Albino akipiga yowe, haraka alikimbilia katika eneo la tukio na kukuta diwani akiendelea kukata kata Ng’ombe wao bila huruma.
“Huku nikipiga yowe, nilimwomba diwani Matheo aache kuwakata ng’ombe na badala yake wamkate yeye hadi afe kwa madai kuwa wanakata Ng’ombe ambao hawana hatia yoyote. Bahati nzuri waliacha zoezi la kukata Ng’ombe wetu”,amesema kwa uchungu mkubwa.
Kwa upande wake mwenye mali hizo shamba la Alizeti na Ng’ombe, John  Theodore Ghumpi amesema siku ya tukio hakuwepo nyumbani alikuwa Singida mjini kikazi.
Amesema alipigiwa simu na kuelezwa juu ya tukio hilo mbaya na hivyo alirudi haraka nyumbani kwake katika kijiji cha Minyinga.
John alisema anahisi diwani Matheo amefanya kitendo hicho kwa makusudi kutokana na ugomvi wao wa kugombe mbuga yenye ukumbwa wa ekari 50.
“Katika ugomvi huu wa muda mrefu,mwaka 1997 hadi 2007,tumekuwa tukifanya kesi katika mahakama mbalimbali na mwaka 2007,tulimshinda katika mahakama kuu Dodoma na aliamriwa kuondoka katika mbuga hiyo”amesema na kuongeza; 
“Cha kusikitisha ni kwamba pamoja na mahakama kuu kutoa amri hiyo halali mwaka 2007 aondoke katika eneo hilo,hadi sasa bado ameng’ang’ania eno letu hataki kuondoka.Tumefanya juhudi kubwa kuomba kuomba mamlaka zinazohusika ikiwa ni pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Singida,lakini hadi sasa juhudi hizo hazijazaa matunda.
Mkulima huyo na mfugaji,alisema jambo jingine linalomsikitisha zaidi ni kauli ya mbunge wa jimbo la Singida mashariki,Tundu Lissu kumpigia simu mkuu wa kituo cha Makiungu akiagiza diwani Matheo Alex aachiwe kwa dhamana na kwamba atamtetea katika kesi ya kukata kata ng’ombe na kufyeka shamba la alizeti.
“Kama kweli yeye Tundu Lissu ni mbunge wa wakazi wa jimbo la Singida mashariki ambaye wajibu wake ni pamoja na kuwaongoza wapiga kura na wananchi, kutenda mambo mema na yanayozingatia sheria, nasubiri kwa hamu kama atabariki kitendo cha diwani Matheo kwa kumtetea katika kitendo chake hiki cha kinyama”,alisema huku machozi yakimtiririka.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa Singida.ACP Geofrey Kamwela alikiri kupokea taarifa ya tukio lililofanywa na diwani Matheo la tuhuma ya kukata kata Ng’ombe sita na kuharibu ekari mbili na nusu za shamba la alizeti.
“Kwa sasa vijana wangu wapo eneo la tukio.Wakishamaliza uchunguzi nitatoa taarifa kamili ili wananchi waweze kujua undani wa tukio hilo mbaya”amesema kamanda huyo wa mkoa.

No comments:

Post a Comment