KUMBE!
Baadhi ya wabunge wa kike ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wanatumia vipodozi vinavyochubua ngozi ya juu ya mwili ili wawe
na mwonekano mweupe (kama wazungu). Kauli
hiyo ya kushangaza ilitolewa bungni Mei 9, mwaka huu na Mbunge wa Nkasi
Kaskazini, Ally Kessy wakati alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu udhibiti wa dawa kwa Mamlaka ya Chakula
na Dawa Tanzania (TFDA).
Akizungumza
bila kupepesa macho, Mheshimiwa Kessy alisema kuwa baadhi ya
waheshimiwa wa kike ndani ya mjengo wanatumia vipodozi ambavyo vina
madhara makubwa kwa afya ya mtumiaji.
Grace Kiwelu.
MSIKILIZE KWA KINA
“Labda niseme tu TFDA wanapaswa kusimamia kuhakikisha vipodozi vyenye
madhara haviingii nchini, watu wengi sana wanaathirika na kupata
magonjwa ya kansa ya ngozi.
“Humu ndani (bungeni) wapo waheshimiwa ambao wanatumia vipodozi hivyo
ambapo wanapokuja kuumwa serikali inapoteza fedha nyingi kwenda
kuwatibia nje ya nchi,” alisema Kessy.
WABUNGE WAMEKASIRIKA?
Habari za ndani zinaweka wazi kwamba, baada ya Mheshimiwa Kessy
kuzungumza madai hayo, baadhi ya waheshimiwa hao wameonesha kukasirishwa
na kauli hiyo wakisema ililenga kuwachafua.
“Kwa kweli waheshimiwa wangekuwa wanachuja cha kuzungumza, mambo mengine
ukiyasikia unapata picha kwamba lengo la msemaji ni kuchafua watu,”
aliweka wazi mbunge mmoja alipoongea na gazeti hili huku akigoma jina
lake lisiandikwe gazetini.
ALICHOSEMA MTAALAM WA AFYA
Baada ya kauli hiyo ya Mheshimiwa Kessy ambayo ndiyo habari ya mjini kwa
sasa, Ijumaa Wikienda lilizungumza na mtaalam wa masuala ya afya ambaye
aliomba hifadhi ya jina lake.
Alibainisha kuwa tatizo litokanalo na matumizi ya vipodozi vikali ni
kubwa sana Bongo na kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele, taifa linazidi
kuangamia kwa ugonjwa wa kansa ambayo husababishwa na kujichubua.
“Serikali kupita mamlaka zinazohusika inapaswa kutilia mkazo suala hili
na kuhakikisha inathibiti mianya yote ya kuingizia madawa haya ambayo
madhara yake ni makubwa kwa taifa, hasa magonjwa ya ngozi kama vile
kansa.
“Hii ni hatari kubwa sana, kwa sababu wabunge ambao ndiyo walipaswa kuwa
mfano wa kuigwa, badala yake wao wenyewe wanadaiwa kuwa watumiaji
wazuri,” alisema mtaalam huyo.
WABUNGE WANENA
Baada ya mtaalam huyo kuweka wazi hali halisi ya madhara ya matumizi ya
madaya hayo, Ijumaa Wikienda lilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya
waheshimiwa wabunge wanawake ambapo kila mmoja alifunguka kivyake:
ZARINA MADABIDA (Viti Maalum CCM)
“Mimi ni Pharmacia (mtayarishaji na mtoaji wa madawa), natambua vema
madhara ya hivyo vipodozi. Sina uhakika kama kuna wabunge wanatumia
lakini kama wapo basi nawashauri waache mara moja.
“Mimi situmii hata kidogo, si unaniona hata rangi yangu ni maji ya kunde ya asili?!”
GRACE KIWELU (Viti Maalum- Chadema)
“Mbunge ni mtu mzima huwezi kumzuia. TFDA wanapaswa kufanya kazi yao ya
udhibiti, kweli wanaofanya hivyo wapo lakini tunapaswa kuwapa elimu.
“Mimi situmii, kuanzia mikono hadi miguu yangu vinafanana. Hakuna ‘pepsi mirinda’ katika mwili wangu.”
SUZAN LYIMO (Viti Maalum-Chadema)
“Wabunge wanapaswa wawe mfano, japo hii ni ishu personal (binafsi)
lakini ni vema basi wakatazama madhara yake. Vipo vipodozi ambavyo
havina madhara na vingine vina madhara.”
CHIKU ABWAO (Viti Maalum-Chadema)
“Wabunge ni watu wazima, kujichubua ni ishu private (siri). Lakini na
yeye Mheshimiwa Kessy kama ameona wabunge wana tatizo hilo anapaswa
kuwashauri waache. Mimi natumia vipodozi lakini visivyo na madhara.”
CATHERINE MAGIGE (Viti Maalum-CCM)
“Ni mambo binafsi, kuhusu wanaotumia mimi sina comments (maoni) yoyote.
Ningekuwa natumia mimi ungeniona vinavyoniathiri, sijawahi kutumia
kabisa jamani.”
ESTER BULAYA (Viti Maalum-CCM)
“Kwanza sikuwepo bungeni siku hiyo mheshimiwa huyo alipotoa hoja yake.
Halafu mimi ni mweusi, huwa sipendi kutumia vipodozi vya kuchubua ngozi
ili niwe mweupe, napaka mafuta ya kawaida kabisa. Urembo wangu mkubwa
mimi upo kwenye nywele.”
ANNA KILANGO (Same Mashariki-CCM)
“Ha! Haa! Haaa! Mimi situmii jamani, rangi yangu mimi ni natural (ya
asili) hakuna mkorogo hata kidogo, sijui kama wapo wanaotumia.”
SARAH MSAFIRI (Viti Maalum-CCM)
“Hivyo vitu vinahitaji utaalam sana kabla ya kutumia, mimi situmii hivyo sina uzoefu wowote labda uwaulize wanaotumia.”
ZAINABU KAWAWA (Viti Maalum-CCM)
“Ni kauli ya kitawala, siwezi kutolea tamko lakini pia madhara ni ya kitaalam.”
MARY MWANJELWA (Viti Maalum-CCM)
“Baadhi ya waheshimiwa walikwazika lakini kiukweli vipodozi hivyo vina
madhara makubwa. TFDA wanapaswa kutoa ufafanuzi juu ya hilo.”
DUKA LATAJWA
Baadhi ya
waheshimiwa waliliambia gazeti hili kuwa, waheshimiwa wanaojichubua
hutumia vipodozi vyenye ‘kaloraiti’ kutekeleza nia yao na kwamba duka
lao kubwa kwa Dar es Salaam lipo Kariakoo kwa jamaa Mkongomani aitwaye
Hashim.
No comments:
Post a Comment